WIZI KWA NJIA YA MTANDAO WATIKISA BENKI RWANDA
Kashfa kubwa ya udanganyifu wa mtandao imetikisa Benki ya Equity nchini Rwanda, na kuchochea msako mkali wa wahalifu wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Wachunguzi wamewakamata jumla ya washukiwa 35, wakiwemo sita waliokamatwa nchini Uganda, huku juhudi zikiendelea kuvunja mtandao uliokuwa ukihusika na wizi wa mamilioni ya fedha kupitia mifumo ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Uchunguzi ya Rwanda, wahalifu hao wanadaiwa kutumia mianya katika mifumo ya benki na huduma za fedha za simu kuhamisha takribani dola milioni 3.4. Kati ya fedha hizo, karibu dola laki tisa zimefanikiwa kupatikana, huku kiasi kikubwa kikiwa bado hakijapatikana.
Benki ya Equity Rwanda imesema mifumo yake ya ufuatiliaji iligundua miamala isiyo ya kawaida na kuchukua hatua za haraka, ambapo miamala mingi ilirejeshwa ndani ya saa 24.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, James Mwangi, amesema hawatavumilia uhalifu wa kifedha na kwamba kila anayehusika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wachunguzi wanashuku kuwa wahalifu walitumia udhaifu katika mifumo ya benki ya kidijitali pamoja na huduma za fedha za simu, ikiwemo kuweka fedha nyingi isivyo kawaida kwenye kadi za SIM, baadhi zikiwa hazijasajiliwa.
Uchunguzi huo pia umevuka mipaka, huku mamlaka za Uganda zikishirikiana na Rwanda kuchunguza tukio hilo na kukusanya ushahidi wa kidijitali.
Wataalamu wanasema tukio hili linaakisi ongezeko la uhalifu wa mtandao katika sekta ya fedha za kidijitali barani Afrika, huku nchi mbalimbali zikichukua hatua za kuimarisha usalama wa mifumo yao.
Nchini Rwanda, serikali imeongeza uwekezaji katika usalama wa mtandao na kuimarisha usimamizi ili kulinda miundombinu ya kifedha.
Udukuzi na udanganyifu wa fedha kwa njia ya kidijitali barani Afrika unaongezeka kwa kasi, ukichochewa na ukuaji mkubwa wa matumizi ya benki za mtandao na huduma za simu. Kwa mujibu wa Interpol, bara la Afrika hupoteza zaidi ya dola bilioni 4 kila mwaka kutokana na uhalifu wa mtandao, ikiwa ni pamoja na wizi wa fedha na ulaghai wa kidijitali. Nchi zinazoongoza kwa visa vingi ni Kenya, Nigeria, na Afrika Kusini kutokana na matumizi makubwa ya huduma za kifedha za kidijitali.
Aidha, Afrika inachangia zaidi ya nusu ya akaunti zote za fedha kwa njia ya simu mobile money duniani, hali inayofanya huduma hizi kuwa shabaha kuu ya wahalifu wanaotumia mbinu kama kubadilisha SIM, ujumbe ulaghai, na udukuzi wa akaunti za benki.

.png)
Post a Comment