MTANGAZAJI

ASHITAKIWA NA SERIKALI KUHUSU SABATO

 


Serikali ya Marekani inamshtaki mmoja wa wamiliki wa leseni za biashara za mgahawa wa chakula wa Chick-fil-A, ikituhumiwa kutekeleza ubaguzi wa kidini baada ya mfanyakazi kudaiwa kunyimwa ruhusa ya kutofanya kazi siku za Sabato.

Tume ya Fursa Sawa za Ajira (EEOC) inasema kuwa meneja mmoja katika biashara ya mgahawa wa  Chick-fil-A huko Austin, Texas, uitwayo “Hatch Trick,” alifutwa kazi baada ya kuomba kutofanya kazi siku za Jumamosi kwa sababu hiyo ndiyo siku ya Sabato kwa dhehebu lake la kidini.

EEOC inasema kuwa alieleza hitaji lake la kutopangiwa kazi siku za Jumamosi kwa sababu za kidini wakati wa mahojiano ya kazi. Inaelezwa kuwa Hatch Trick mwanzoni iliheshimu ombi lake, lakini baadaye ilianza kumpanga kufanya kazi siku za Jumamosi.

Alikata rufaa kwa uongozi na kupendekeza njia mbadala ili aweze kuendelea na kazi yake ya usimamizi huku akiendelea kushika Sabato ya Jumamosi, lakini EEOC inasema Hatch Trick ilimwambia atalazimika kuchukua kazi yenye mshahara mdogo pamoja na saa chache za kazi na marupurupu machache. Alipokataa, alifutwa kazi.

EEOC inadai kuwa Hatch Trick ilikiuka sheria ya haki za kiraia ya mwaka 1964 kwa kushindwa kutoa mazingira ya kazi yanayokubaliana kwa kiwango kinachofaa na imani ya kidini ya mfanyakazi huyo.

Hatch Trick na Chick-fil-A bado hawajatoa tamko rasmi kuhusu kesi hiyo. Chick-fil-A inakadiliwa kuwa na migahawa 3,000 katika zaidi ya majimbo 48 ya Marekani pamoja na Washington, D.C. na Puerto Rico, huku Texas ikiwa jimbo lenye matawi mengi zaidi.

Kesi za ubaguzi wa kidini mahali pa kazi zimekuwa zikiongezeka nchini Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa Tume ya Fursa Sawa za Ajira (EEOC), maelfu ya malalamiko yanayohusiana na dini huwasilishwa kila mwaka, yakihusisha waajiri kushindwa kuheshimu siku za ibada, mavazi ya kidini, au desturi za waumini. 

Kampuni kadhaa zimelazimika kulipa fidia kubwa baada ya wafanyakazi kudai kunyimwa haki zao za kidini. Mwaka 2023 kampuni moja ya usafirishaji ilikubali kulipa mamia ya maelfu ya dola baada ya mfanyakazi wa Kiislamu kudai kunyimwa nafasi ya kuswali kazini, huku kesi nyingine zikihusisha wafanyakazi wa Kikristo, Wayahudi, na wa Sabato waliodai kuadhibiwa kwa kushindwa kufanya kazi siku zao za ibada. 

Wataalamu wa sheria za ajira wanasema ongezeko hilo linaonyesha umuhimu wa waajiri kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa wafanyakazi wenye mahitaji ya kidini kwa mujibu wa sheria za Marekani.

 Maduka mengi ya Chick-fil-A hufungwa Jumapili kutokana na misingi ya kidini ya mwanzilishi wa kampuni hiyo, S. Truett Cathy. Tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa mwaka 1946, sera hiyo imekuwa ikilenga kuwapa wafanyakazi muda wa kupumzika, kuwa pamoja na familia zao, na kushiriki shughuli za ibada siku hiyo. Chick-fil-A imeendelea kushikilia utamaduni huo wa kufunga Jumapili licha ya ushindani mkubwa katika sekta ya migahawa ya chakula cha haraka nchini Marekani.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.