MTANGAZAJI

SELFIE ILIYOACHA MAJONZI

 


Saa chache kabla ya janga kubwa kutokea, picha ya selfie iliyojaa tabasamu na matumaini ilichukuliwa ikiwa ni kumbukumbu ya matumaini, upendo, na mwanzo mpya. Katika picha hiyo ambayo sasa "imeganda"  ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari duniani inamwonesha Dkt. Pratik Joshi, mkewe Dkt. Komi Vyas, na watoto wao watatu wadogo waliokuwa ndani ya ndege ya Air India AI-171, wakielekea kuanza maisha mapya pamoja jijini London,Uingereza. 

Inaelezwa na vyombo vya habari vya India kuwa ndege hiyo ilianguka katika eneo la makazi huko Ahmedabad sekunde 32 baada ya kupaa, Juni 12,2025  na kuua wanafamilia wote watano na abiria wengine.

Ajali hiyo, ambayo imegharimu maisha ya watu 242 waliokuwa ndani ya ndege, imeacha jeraha lisilosahaulika kwa jamii za Banswara na Udaipur huko Rajasthan, ambako baadhi ya wahanga walitoka. 

Kati ya simulizi zote za huzuni, habari ya familia ya Joshi imesimama kama mfano wa maumivu ya kupoteza ndoto kwa ghafla kama ilivyothibitishwa na News18.

Dkt. Pratik Joshi alikuwa akiishi London kwa miaka sita, akiweka msingi wa kazi na maisha ya baadaye. Mkewe, Dkt. Komi Vyas, ambaye alikuwa Daktari mashuhuri katika Hospitali ya Pacific mjini Udaipur, alijiuzulu kazi yake siku mbili tu kabla ya safari hiyo, akiwa tayari kuhamia na kuungana tena na familia yao kwa kudumu. Watoto wao mapacha wa kiume Nakul na Pradyut, wenye umri wa miaka mitano, pamoja na binti yao Miraya, mwenye miaka minane walikuwa na shauku kubwa ya kuanza maisha mapya ughaibuni. 

Pratik Joshi akiwa mtaalamu wa programu za kompyuta, kwa muda mrefu alikuwa akiota ndoto ya kujenga maisha bora ughaibuni kwa ajili ya mke wake na watoto wao watatu. Mizigo ilikuwa imefungwa, kwaheri zimesemwa, na maisha mapya yalikuwa yanawasubiri katika nchi ya ng'ambo.

Wakiwa na matumaini, furaha, na mipango, walipanda ndege hiyo kuelekea London. Walipiga “selfie” hii, wakaituma  kwa ndugu. Lakini hawakuwahi kufika.

Kwa muda wa sekunde chache, ndoto za maisha yote ziligeuka kuwa majivu. Ni ukumbusho wa kikatili kwamba maisha ni dhaifu sana. Kila kitu unachojenga, kila unachokitamani, kila unachokipenda vyote vinaning’inia kwa uzi mwembamba.

Maisha ni zawadi isiyodumu yanaweza kubadilika kwa sekunde chache tu. Habari ya familia ya Joshi ni ukumbusho wa kina kwamba hatuishi milele, lakini tunayo nafasi ya kuishi kwa upendo, imani, na umoja kila siku. Ingawa safari yao ilikatika ghafla, upendo wao, ndoto zao, na tabasamu zao vinabaki hai mioyoni mwa wote waliowapenda. Waliondoka wakiwa na tumaini, wakitazama mbele kwa maisha mapya..

Kila mmoja wetu aliye bado na pumzi ya uhai tupendane  kwa dhati, tusamehe kwa haraka, tuishi kwa shukrani. Maisha ni safari fupi.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.