VISA ZA MAREKANI KWA WANAFUNZI ZAREJEA KWA MASHARTI ZAIDI
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuanza tena rasmi mchakato wa utoaji wa visa kwa wanafunzi wa kimataifa waliokuwa wakisubiri kujiunga na taasisi mbalimbali za elimu nchini humo.
Hata hivyo, hatua hiyo sasa inakuja na masharti mapya, ambapo waombaji wote wanatakiwa kufungua akaunti zao za mitandao ya kijamii kwa uchunguzi wa serikali.
Kwa mujibu wa tangazo la Juni 18,2025 wanafunzi wote wanaotuma maombi ya visa sasa watalazimika kuweka mitandao yao ya kijamii katika hali ya “public” ili kurahisisha ukaguzi wa kina na maafisa wa ubalozi.
Serikali inasema hatua hiyo inalenga kubaini maudhui yoyote ya uhasama dhidi ya Marekani, taasisi zake, tamaduni au misingi ya taifa hilo.
Wizara imesema kwamba mtu yeyote anayekataa kuweka wazi mitandao yake ya kijamii anaweza kuonekana kama mtu anayejaribu kuficha jambo, hivyo maombi yake yaweza kukataliwa.
Wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali kama China, India, Mexico na Ufilipino wamekuwa wakisubiri kwa hamu kufunguliwa kwa ratiba mpya za mahojiano ya visa. Mwanafunzi mmoja wa shahada ya uzamivu kutoka Toronto, mwenye asili ya China, amesema amefanikiwa kupata nafasi ya mahojiano wiki ijayo na anatarajia kuanza kazi ya utafiti nchini Marekani mwishoni mwa mwezi Julai.
Lakini mashirika ya kutetea haki za kiraia yamepinga hatua hiyo. Jameel Jaffer, mkurugenzi wa Taasisi ya Knight First Amendment katika Chuo Kikuu cha Columbia, amesema:
“Sera hii inamfanya kila afisa wa ubalozi kuwa mchunguzi wa kisiasa, jambo litakalozuia uhuru halali wa kujieleza duniani kote.”
Kwa miezi ya hivi karibuni, wanafunzi wa kimataifa wamekuwa wakikumbwa na mashinikizo kadhaa. Serikali ya Trump imewahi kufuta vibali vya wanafunzi waliokuwa na makosa madogo, kabla ya kubadili uamuzi huo.
Aidha, utawala huo umetishia kuzuia wanafunzi wa kigeni kujiunga na taasisi kama Harvard, ukitaka vyuo nchini humo kupunguza idadi ya wanafunzi wa kimataifa hadi asilimia 15 pekee.
Katika hatua nyingine, Marekani imezitaka nchi 36 kuboresha mifumo yao ya uchunguzi wa wasafiri ndani ya siku 60 au zikabiliane na marufuku ya kusafiri kwenda Marekani, ambayo tayari inahusisha mataifa 12.
Post a Comment