MTANGAZAJI

MIKAKATI YA TANZANIA YA "KIDIGITI"

 

Watendaji wa Taasisi za umma na binafsi nchini Tanzania  ambao wanatekeleza ajenda ya kuipeleka nchi hiyo  katika uchumi wa kidijiti wametakiwa kushirikiana na kutekeleza jukumu hilo kwa weledi na ubora wa viwango vya Kimataifa.

Akizungumza katika Jukwaa la Nne la Ubunifu na Teknolojia lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania  Dkt. Jim Yonazi amesititiza ushirikishaji baina ya sekta ya umma na binafsi ili kutimiza malengo ya kuwa na Tanzania ya Kidijiti tunayoihitaji kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema kuwa, kuna fursa nyingi za kiuchumi katika ulimwengu wa kidijiti na Wizara hiyo ipo tayari kupokea na kufanyia kazi maoni ya wadau wa sekta ya umma na binafsi kuhusu nini kinahitaji maboresho katika kufikia dira na malengo ya Taifa ya kuijenga Tanzania ya Kidijiti.

Dkt. Yonazi amezungumzia juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayoendesha uchumi wa kidijiti kwa kuongeza wigo wa usambazaji wa miundombinu na ufikishaji wa huduma za TEHAMA nchini.

“Kama mnavyofahamu hivi karibuni kupitia Shirika letu la Mawasiliano la TTCL tumefikisha intaneti yenye kasi katika Mlima Kilimanjaro na mradi wa kufikisha intaneti majumbani “fiber to home” tayari umeanza kutekelezwa na TTCL lengo ni kufikia uchumi wa kisasa wa kidijiti katika nchi yetu”, amesema Dkt. Yonazi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amesema kuwa Jukwaa la Ubunifu na Teknolojia limewakutanisha wataalamu wabobezi, watafiti, wabunifu na watunga sera ili kujadili na kutoka na taswira tofauti ya kuijenga Tanzania ya Kidijiti kwa kuangazia vipaumbele na mahitaji ya watanzania.

Jukwaa hilo la Nne la Ubunifu na Teknolojia lilikuwa na kauli mbiu ya Tanzania ya Kidijitali Tunayoihitaji, Hatua zipi zichukuliwe Kuifikia? liliandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia programu ya ubunifu ya FUNGUO na kuwakutanisha wadau wa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  kutoka taasisi za umma na binafsi nchini Tanzania.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.