MCH GEOFFREY MBWANA AWEKA REKODI KATIKA KANISA LA WA ADVENTISTA
Mch Geoffrey Gabriel Mbwana ameingia katika rekodi za Kanisa la Wa Adventista wa Sabato kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Makamu wa Kiongozi wa Kanisa la Wa Adventista wa Sabato Ulimwenguni kwa mihula mitatu akiwa yalipo makao makuu ya Kanisa hilo Silver Spring,Maryland,Marekani.
Mbwana ametangazwa na kupitishwa kushika nafasi hiyo kwa miaka mitatu ijayo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 61 wa Konferensi Kuu ya Kanisa hilo ulimwenguni uliofanyika St Louis,Missouri Marekani.
Kanisa la Wa Adventista wa Sabato hufanya mkutano wake Mkuu wa Konferensi kuu kila baada ya miaka mitano na huwakutanisha wajumbe wake kutoka nchi mbalimbali Duniani lilipo kanisa hilo mbapo mwaka huu idadi ya wajumbe walipangwa kuhudhuria ni 2672 na wengine 567 kupitia mtandao wa zoom.
Mkutano wa mwaka huu unafanyika baada ya kuahirishwa mara mbili kutokana na janga la Uviko-19 lililotokea katika nchi mbalimbali Duniani.
Mchungaji Mbwana anaungana na Makamu wa Kiongozi wa Kanisa hilo sita ambao ni Guillermo E. Biaggi,Abner De Los Santos,Artur Stele,Thomas Lemon,Audrey Andersson na Maurice Valentine
Geoffrey Gabriel Mbwana alichaguliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi hiyo mwaka 2010 akitokea katika Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) ambako alikuwa Kiongozi wa Kanisa la Wa Adventista wa Sabato ukanda huo wenye nchi 11,kuanzia mwaka 2003.
Kabla ya Kuongoza Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) Mch Mbwana amewahi kuwa Kiongozi wa Konferensi ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania (NETC) na kisha Kiongozi wa Kanisa la Wa Adventista wa Sabato Tanzania ambapo kulikuwa na Union moja nchini humo kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2002.
Alizaliwa Oktoba 20, 1955 nchini Tanzania, Mbwana amewahi kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari na Chuo na alifanya kazi ya Uinjilisti wa Vitabu nchini India na Sweden.
Mbwana alihitimu Shahada yake ya kwanza ya Elimu ya Dini na Saikolojia kutoka katika Chuo Kikuu cha Spicer kilichoko India mwaka 1982,Alipata Shahada ya Uzamili katika ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Andrews Marekani mwaka 1984 na alihitimu Shahada ya Uzamili ya Saikolojia ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Poona mwaka 1986.
Mchungaji Mbwana na mkewe Nakku wana watoto wawili ambao ni Orupa na Upendo.
Post a Comment