MTANGAZAJI

KAMATI YA WIZARA YA FEDHA YATAKIWA KUTOA TAARIFA SAHIHI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu ameitaka kamati ya Mawasiliano ya Wizara hiyo kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma kwa kuwa ni haki ya wananchi kupata taarifa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

 

Agizo  hilo limetolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lusius Raphael Mwenda, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kamati ya Mawasiliano ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyowakutanisha wajumbe kutoka kwenye Idara na Vitengo vya Wizara hiyo wakati wa kikao kazi, mjini Morogoro.

 

Amesema Kamati ya Mawasiliano ni kiungo muhimu cha masuala ya mawasiliano kati ya Idara/Vitengo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, ambacho ndicho kimepewa majukumu ya kuwasiliana na wadau wetu muhimu wanaotarajia au wanaotegemea kupata taarifa kutoka kwenye kamati kwa ajili ya matumizi yao mbalimbali yakiwemo ya kiutafiti.

 

Alisema kuwa miongoni mwa kazi ya kamati hiyo ni pamoja na kuratibu taarifa zinazohusu Kitengo au Idara, kukusanya na kuandaa taarifa zinazopaswa kutolewa kwa Umma na kuziwasilisha Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kuandaa taarifa za utekelezaji na kuandaa taarifa za zitakazotumika katika majarida, vipeperushi na mabango.

Aidha pamoja na majukumu waliyopewa kamati hiyo, ametoa angalizo la kufuata utaratibu wa kutoa taarifa kwa kuwa kuna watu maalumu waliopewa kibali cha kufanya kazi hiyo kwenye Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ambapo kwa upande wa Wizara waliopewa jukumu hilo ni Katibu Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye pia ni Msemaji wa Wizara hiyo.

 

 Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja aliahidi kusimamia kamati vizuri na kutoa mrejesho kwa ngazi husika, pia alieleza kuwa wajibu wa kamati ni kuisogeza Wizara karibu ya wananchi na washirika wa maendeleo ili wajivunie uwepo wa Wizara kwa wao kupata habari za kweli zitakazotolewa kwa wakati ili wazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa.

 


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.