NEMC YASISITIZA MARUFUKU YA VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI VISIVYOKIDHI VIWANGO
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) limewataka wananchi kutojihusisha na utengenezaji, usambazaji, uuzaji au utumiaji wa mifuko na vifungashio vya plastic visivyokidhi viwango kwa mujibu wa Sheria, kwani kufanya hivyo ni kosa la Kisheria.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Bi. Redempta Samwel kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Kisutu na Machinga Jijini Dar es salaam.
Katika ziara yake amebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanajihusisha na uuzaji na usambazaji wa mifuko na vifungashio vya plastiki visivyokidhi vigezo.
Bi. Redempta Samweli amesema baada ya kufanya ukaguzi, viroba zaidi ya hamsini vyenye vifungashio vya aina mbalimbali visivyokidhi viwango vimekamatwa na vitaharibiwa na hatua zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaohusika.
Kufuatia changamoto hiyo, amewaambia watanzania kuwa ni marufuku kutengeneza, kusambaza, kuuza au kutumia mifuko na vifungashio hivyo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Sheria.
“Tumefanya kaguzi na kukamata viroba zaidi ya hamsini vyenye vifungashio vya aina mbalimbali vinavyotengenezwa hapa nchini visivyokidhi viwango. Viroba hivi vitaharibiwa na hatua kali za Kisheria zitachuliwa dhidi ya wanaohusika na zoezi hili ni endelevu.
Sheria ya Mazingira na Kanuni ya kudhibiti mifuko ya plastiki ya mwaka 2019 ni marufuku kutengeneza, kusambaza, kuuza au kutumia vifungashio visivyokidhi viwango, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Kanuni ya katazo la mifuko ya plastiki.
Sambamba na hilo Bi. Redempta Samwel, amewataka watanzania kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni ili kuepuka migogoro na Serikali na kuepuka gharama zisizokua za lazima.
“Niwaombe watanzania wote kwa ujumla, tutumie mifuko mbadala na vifungashio vilivyoruhusiwa Kisheria na vyenye viwango ili kuepuka migogoro na Serikali na kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.”
Naye Bw. Hamadi Taimuru Kissiwa Meneja Kanda ya Mashariki Kusini ameendelea kuwaasa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutokuzalisha, kutokupokea, kusambaza na kutumia mifuko na vifungashio visivyokuwa na viwango.
Anasema watengenezaji wa vifungashio visivyokua na viwango hawalipi kodi na vifungashio hivyo vinauzwa kwa bei ya chini.
Post a Comment