WANANCHI MULEBA HAWANA MAWASILIANO YA SIMU NA REDIO ZA TANZANIA
Wananchi wa Wilaya ya Muleba nchini Tanzania wamesema hawana huduma ya mawasiliano ya simu ya Redio za Tanzania hasa Redio ya Taifa TBC na matokeo yake wanasikiliza redio za nchi jirani ya Rwanda hivyo kushindwa kuelewa kinachoendelea ndani ya nchi yao.
Wananchi hao wamemueleza masikitiko yao Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Mhandisi Kundo Mathew alipofanya ziara wilayani humo hivi karibuni.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyo imeshaanza mchakato wa kuanzisha redio ya jamii lakini mchakato umekuwa mrefu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivyo kumuomba Naibu Waziri huyo kuingilia kati suala hilo ili redio hiyo ianzishwe na kuanza kuwahudumia wananchi wa Muleba.
Mhandisi Kundo alifanya ufuatiliaji wa hatua iliyofikiwa kupitia Mkuu wa Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo aliyeambatana nae katika ziara hiyo ambapo alimpigia simu Afisa anayeshughulikia maombi hayo wa TCRA Makao Makuu ambaye alitolea ufafanuzi kuwa maombi rasmi bado hayajafika katika ofisi hizo lakini Afisa wa Halmashauri ya Muleba alifika akiwa na mshauri wake na akamuelekeza namna ya kuandaa andiko la maombi hayo na mpaka sasa bado hayajawasilishwa.
Mhandisi Mihayo alitolea ufafanuzi wa suala hilo kwa kuzungumzia umakini wa TCRA katika mchakato mzima wa kutoa leseni ya kuanzishwa kwa redio yeyote nchini ambapo alisema kuwa Afisa wa Halmashauri hiyo alitakiwa kufika kwenye ofisi za TCRA Kanda ya Ziwa ili kupata ushauri na huduma ya kuanzisha redio hiyo badala ya kwenda moja kwa moja Makao Makuu ya TCRA Dar es Salaam.
Mhandisi Kundo ametoa maelekezo kwa Mamlaka hiyo kuhakikisha inaharakisha mchakato wa kutoa leseni ya kuanzishwa kwa redio hiyo pindi maombi rasmi yakiwafikia.
Katika hatua nyingine Mhandisi Mihayo amesema kuwa taratibu za kuweka mitambo ya kuongeza usikivu wa redio ya TBC katika maeneo ya Kanda ya ziwa hasa mipakani zinaendelea ikiwa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Muleba ikiwemo Kijiji cha Kakoma ifikapo Oktoba 2021.
Kwa upande wa mawasiliano ya simu Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard amesema kuwa amepokea mahitaji ya wananchi wa Muleba na Mfuko huo utavijumuisha vijiji vyenye changamoto ya mawasiliano katika zabuni zao ikiwa ni muendelezo wa kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini na mipakani
Post a Comment