VITA DHIDI YA UKATILI IANZIE NGAZI YA FAMILIA
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu
amesema zinahitajika mbinu shirikishi kuanzia ngazi ya Familia za
kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mimba za utotoni.
Dkt.
Jingu ameyasema hayo Jijini Dodoma katika kikao chake na Wajumbe wa
Mtandao wa kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania TECMN ikiwa ni njia ya
kupambana na vitendo vya ukatili.
Amesema
mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia zikiwemo ndoa za utotoni
yanatakiwa kuanza katika ngazi ya familia na hatimaye mifumo yake
kuendelea hadi taifa.
Akitoa
mifano katika baadhi ya mikoa, Katibu Mkuu Jingu amesema pamoja na
jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kusimamia sheria za
kuharamisha vitendo hivyo, bado vitendo hivyo vinaendelea kutokana na
mila na desturi za jamii husika.
Amesema
baadhi ya ndugu na wanafamilia wanachelea kutoa ushahidi wa unyanyasaji
kutokana na ukali wa sheria zilizopo ili kuwanusuru wanafamilia
wanaohusika katika vitendo hivyo vya ukatili ikiwa ni pamoja na
kuwakatili watoto kwa kuwapa mimba.
Akizungumzia
njia za mapambano dhidi ya ukatili huo, Katibu Mkuu amesema mkakati wa
kuboresha uchumi wa kaya kwa kuwawezesha wanawake kushiriki katika
uzalishaji mazao ya kimkakati hivyo kuimarika kiuchumi na kushiriki
kuzitunza familia zao.
Ameshauri
kampeni za kukomesha ukatili zifanyike kwa kushirikisha vyombo vya
habari na watu wenye ushawishi katika jamii husika wakiwemo viongozi wa
dini ili kuwezesha jamii kutambua tatizo na kuchukua hatua za kulikataa.
Amefafanua
kuwa kuna hatua zilizochukuliwa kupitia Mpango kazi wa taifa wa
kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto MTAKUWWA kuanzia ngazi za
chini lakini bado jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha kamati hizo
zinafanya kazi kwa ufanisi.
Ameongeza
kuwa ni muhimu kuwa na vituo vya malezi na makuzi ya awali ya watoto
katika jamii ili waweze kujihusisha na mambo yanayoweza kuwakuza kiakili
badala ya kuachwa bila uangalizi na hatimaye kujikuta katika mazingira
hatarishi.
Mtandao wa TECMN unajumuisha Mashirika 64 Yasiyo ya kiserikali ambao unafanya kazi katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Post a Comment