NAIBU WAZIRI MWANAIDI ATAKA ULINZI KWA WANAWAKE NA WATOTO DHIDI YA VITENDO VYA UKATILI
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Mwanaidi Ali Khamis amewataka
watendaji wanaosimamia utekelezaji wa Sheria ya ulinzi wa haki za
wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili kuhakikisha haki
inapatikana ndani ya kipindi kilichowekwa na ikiwezekana ipatikane kwa
haraka zaidi.
Naibu
Waziri Mwanaidi amesema hayo, Wilayani Kasulu mkoani Kigoma alipofika
katika nyumba moja ya kuwahifadhi wanawake na watoto waliokumbana na
vitendo vya ukatili katika jamii kwenye nyumba salama ya Wote Sawa
iliyoko Wilayani humo.
Naibu
Waziri Mwanaidi amesema kuwa jamii inatakiwa kutoa taarifa dhidi ya
vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia hususan kwa wanawake na watoto ili
kuwawezesha wahanga wa vitendo hivyo kupata haki yao.
“Serikali
inaandaa mazingira ya kukabiliana na vitendo ya ukatili dhidi ya
wanawake na watoto, kwa hiyo msikae kimya dhidi ya ukatili wa vitendo
hivyo, Tumieni mifumo iliyopo kutoa taarifa na Sheria iweze kuchukua
mkondo wake na wahanga hao kupata haki”alisema Niabu Waziri Mwanaidi.
Vilevile
amesema kuwa ukimya katika jamii dhidi ya vitendo hivyo una madhara
makubwa kwa waathirika na wakati mwingine ukimya huo unasababisha
kutoweka kwa ndoto za waathirika katika maisha yao baadaye kutokana na
kuathirika kimwili na kisaiklojia.
Amependekeza mifumo iliyopo katika kusimamia na kuchunguza mashauri ya
unyanyasaji wa kijinsia kuangaliwa upya kwa kuwa muda uliowekwa ni
mwingi ilhali wahanga wanakuwa wakiteseka kwa muda mrefu kabla ya
mashauri hayo kufanyiwa kazi kikamilifu na kufikishwa mahakamani.
Akizungumza
kuhusu uendeshaji wa nyumba salama ya Wote Sawa, Meneja wa nyumba hiyo
Jaqueline Ngalu amesema hatua iliyofikiwa ni kutokana na Serikali kwa
kushirikiana na wadau kuandaa mwongozo wa kitaifa kuanzisha na kuendesha
nyumba Salama.
Post a Comment