MTANGAZAJI

WANANCHI WASISITIZWA KUFANYA UHAKIKI WA LAINI ZA SIMU

 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  Dkt. Faustine Ndugulile
ametoa rai kwa wananchi nchini humo kuendelea kufanya uhakiki wa laini za simu kwa lengo la kutambua laini zilizosajiliwa kwa majina yao ili kuepuka kuhusishwa na makosa ya utapeli mitandaoni.

Hayo ameyazungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa tovuti na Mpango mkakati waWizara hiyo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26 uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi kuepuka kusajili laini kwa kuweka alama ya kidole zaidi ya mara moja ili kuzuia usajili wa laini nyingine za ziada ambazo zinaweza kutumika kufanya uhalifu mitandaoni.

“Wananchi wengi wamekuwa wahanga wa utapeli mitandaoni hivyo Wizara
imejipanga kuimarisha mifumo ya kulinda faragha na taarifa binafsi ili zisitumike
vibaya na watu wasiokuwa na nia njema”, alizungumza Dkt. Ndugulile.
 
 Kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ( TCRA) hadi Januari 12, 2020 kati ya laini milioni 48 zilizosajiliwa nchini,Tanzania  ni laini milioni 26 pekee zilizosajiliwa kwa alama za vidole. 
 
Hata hivyo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ilieleza kuwa  hadi Januari 15, 2020 zaidi ya namba za utambulisho milioni 6 zilizozalishwa, zilikuwa bado hazijatumika kusajilia laini za simu nchini Tanzania.

Aidha, amewaasa wananchi kuacha kutoa taarifa binafsi au kufuata maelekezo
yeyote kwa watu wanaopiga simu na kujitambulisha wanatoka dawati la huduma
kwa mteja katika makampuni ya simu ili kuepuka kutapeliwa.

Ameongeza kuwa namba wanayotakiwa kupigiwa na makampuni ya simu ni namba
100 na sio kupigiwa na namba kutoka mitandao tofauti na mitandao wanayotumia
huku wakijitambulisha wametoka huduma kwamteja na kuomba taarifa zao za
kifedha au kutaka kujua salio lililopo katika laini zao za simu.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.