AGIZO LA TOZO KWA WAMILIKI WA SIMU TANZANIA
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa muda wa siku 14 kuanzia Julai Mosi 1 hadi 15 Julai, 2021, kwa watoa
huduma wote wa Mitandao ya Simu kurekebisha mifumo yao na kuanza kutoza rasmi
makato ya kodi ili Serikali ianze kukusanya fedha ambazo amesema zitatumika
kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuwakwamua wananchi kutoka katika adha mbalimbali.
Nchemba ametoa agizo hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Chama cha Watoa Huduma wa Simu Tanzania (TAMNOA), na kuwaeleza kuwa kodi ya miamala ya simu na bando za mitandao inayotakiwa kuanza kutozwa na mitandao ya simu inalenga kila Mtanzania kuchangia mapato ya Serikali kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Kampuni
za simu msichukulie makato haya kama kodi nyingine mnazowatoza wateja wenu bali
Serikali iliamua kuweka makato haya kwenye miamala ya kuweka muda wa maongezi
na kufanya miamala kwa njia ya simu ili kuwafanya Watanzania na watumiaji
wengine wa simu kuchangia maendeleo ya nchi”alisisitiza Dkt. Nchemba.
Kwa
upande wao Chama cha Watoa huduma za mitandao ya simu, waliiomba Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iwape muda wa kurekebisha mifumo yao
itakayotumika kukusanya tozo hizo kwa kuwa zoezi hilo linahitaji muda wa
kiufundi.
Akizungumza
kwa niaba ya Chama hicho, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Simu ya Vodacom
Bi. Roselynn Mworia, alisema kuwa chama chao kimeupokea mpango huo kwa mikono
miwili na kuwataka wateja wao kuiunga mkono Serikali kwa kuendelea kutumia
huduma za kupiga simu na kufanya miamala ya simu.
Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi karibuni, lilipitisha tozo ya kuanzia
shilingi 10 hadi shilingi 10,000 kutozwa katika kila muamala wa kutuma au
kupokea pesa na kiwango cha shilingi 10 hadi 200 kwa siku kila mteja
anapoongeza salio la muda wa maongezi kwenye simu ambapo kwa pamoja, Serikali
inatarajia kukusanya wastani wa shilingi trilioni1.7 kwa mwaka.
Post a Comment