MFUMUKO WA BEI NCHINI TANZANIA
Mfumuko wa Bei wa Taifa nchini Tanzania kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2021 umefikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2021.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za jamii, Bi. Ruth Minja Mei 10, 2021 jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Ameeleza kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia mwezi Aprili, 2021 iliongezeka kidogo ikilinganishwa na ilivyokuwa Machi, 2021.
“Kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2021 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2021 ikilinganishwa na bei za Aprili, 2020”, alisisitiza Bi. Ruth.
Akifafanua, amesema kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Aprili, 2021 ikilinganishwa mwezi Aprili, 2020 ni pamoja na; ngano kwa asilimia 8.9, nyama asilimia 4.2, samaki wabichi asilimia 28.1, dagaa wakavu asilimia 22.0, mafuta ya kupikia asilimia 24.6, matunda asilimia 24.6, viazi mviringo asilimia 5.7, viazi vitamu asilimia 14.7, ndizi za kupika kwa asilimia 7.6, maharage kwa asilimia 6.4 na mihogo mikavu kwa asilimia 18.7.
Kwa upande wa nchi jirani ya Kenya mfumuko wa bei kwa mwezi Aprili ni asilimia 5.76 ikilinganishwa na asilimia 5.90 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2021.
Kwa upande wa Uganda mfumuko wa bei umepungua hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2021 baada ya nchi hiyo kufanya marejeo ya mfumuko wa bei.
Post a Comment