MTANGAZAJI

VIJANA TANZANIA WATAKIWA KUWA WABUNIFU KATIKA KUTIMIZA NDOTO ZAO


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania  Innocent Bashungwa amewataka vijana nchini humo kuwa wabunifu,wawajibikaji katika kutimiza malengo ya ndoto zao huku akiahidi kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia  na kuratibu vyema shughuli za ubunifu kwa vijana kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.


Waziri Bashungwa ameyasema hayo Februari 04, 2021 alipokua akifungua Kongamano la I HAVE A DREAM  kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Mkoa wa Dodoma lililofanyika ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma.

"Wizara inaweka mazingira mazuri kwa wabunifu ili waweze kufanya kazi za ubunifu katika maeneo waliyopo na kutimiza ndoto zao"alisema  Bashungwa

Bashungwa ameongeza kuwa lengo la Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, la kuihamisha Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara hiyo ni ili isimamie vyema kazi za wasanii ambao ndio wadau wakubwa.


"Kila mtu ana ndoto ambayo anatakiwa aitimize katika umri alionao na umri ujao auwekee malengo ya kuendeleza ndoto hiyo" Mhe. Bashungwa.


Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa kila mtu yupo duniani kwa ajili ya jambo fulani hivyo ni vizuri kila mtu akawajibika katika kufanikisha jambo hilo.


Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Patrobas Katambi akitoa mada katika Kongamano hilo amesema kuwa hakuna kitu kigumu kinachorudisha nyuma mafanikio kama kuwa na woga na hofu, hivyo lazima vijana watambue hilo.


 "Simama katikati ya watu wote ili wakuone una nini cha tofauti na wao na uonyeshe kwa vitendo kitu hicho" alisema Katambi.


Erick Shigongo Mbunge wa Buchosa amesema kuwa safari ya mafanikio inaanza kidogo kidogo kwa kujifunza kila kitu bila kukata tamaa na hatimaye kupata  mafanikio binafsi hatimaye kwa Taifa, ambapo amewasihi vijana kuwajibika katika kutimiza malengo yao.

Mjasiriamali Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole amewashauri vijana kutumia muda vizuri katika kubadili maisha yao, huku msanii Kala Jeremia akisisitiza kuwa kila ndoto lazima iambatane na malengo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.