MTANGAZAJI


Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imetoa agizo kwa wadau wa kazi za Sanaa kuacha kurudia kazi za msanii bila ridhaa au makubaliano na mmiliki wa kazi hiyo.

Wito huo umetolewa hivi karibuni Jijini Dodoma na Afisa Sheria wa Taasisi hiyo Bw. Zephania Lyamuya alipomaliza kusuluhisha mgogoro wa kurudiwa wimbo uitwao “Mungu Baba” wa Bi. Upendo Nkone  uliorudiwa na Studio ya Dom -Tune bila ridhaa ya msanii huyo.

Akizungumza katika kikao hicho Afisa Sheria huyo amesema kazi yoyote ambayo imesajiliwa katika Taasisi hiyo tayari ina Hakimiliki hivyo sio ruhusa kwa mtu yeyote kuitumuia bila makubaliano na mmiliki.

“Natoa wito kwa Wadau wa Sanaa kusajili kazi zao COSOTA ili watambulike na kulindwa kisheria, pia waje kupata elimu ya haki za kazi zao ili kuepuka migogoro isiyokua na ulazima” alisema Bw. Lyamuya.

Kwa upande wake, Msanii Upendo Nkone ameishukuru COSOTA kwa kumsaidia kupata haki katika kazi yake ambayo ilirudiwa bila ridhaa yake huku akitoa wito kwa jamii  kuacha kurudia kazi zake bila ridhaa yake kwakua kazi zake zinalindwa kisheria kwakuwa amezisajili, na kwamba amewaasa wasanii kujisajili BASATA na kusajili kazi zao COSOTA kwa sababu vyombo hivyo vinawatetea wasanii.

Vile vile Muandaaji katika Studio ya DOM –TUNE Bw. Kassim Ally amekiri kufanya makosa hayo na kwamba ameahidi kuheshimu maridhiano yaliyofikiwa huku huku akiishukuru COSOTA kwa kumueleza utaratibu unaopaswa kufuatwa iwapo atahitaji kurudia kazi za msanii yeyote.

Kikao hicho kimemalizika kwa maamuzi kwamba Studio ya DOM- TUNE ifute wimbo wa msanii huyo  katika mitandao ya kijamii  na kulipa fidia ya kiasi cha fedha walichokubaliana ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.