MTANGAZAJI

TPC ONGEZENI MATUMIZI YA TEHAMA KUHUDUMIA WATEJA-WAZIRI Uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) umetakiwa kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili  kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Agizo hilo limetolewa na  Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Dkt. Faustine Ndugulile wakati akifungua mkutano wa 27 wa Baraza
Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania lililofanyika Dodoma. 

Amefafanua kuwa hivi sasa dunia ipo kiganjani na inatumia TEHAMA na maisha yanakwenda kidijitali hivyo TPC nayo iongeze matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wateja kwa kuwa kwa kufanya hivyo TEHAMA itaongeza mapato ya Shirika na kuongeza gawio lake kwa Serikali.


“Sitarajii kuona TPC inaendeshwa kwa hasara, tumieni rasilimali za Shirika kwa ajili ya ustawi wa Shirika na sio ustawi wa mtu binafsi”, amesisitiza Dkt. Ndugulile.


Naye Postmasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe
amesema kuwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi watakuwa na kikao cha siku tatu ambapo watajadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Shirika kwa mwaka 2021/2022; matumizi ya mifumo mipya ya kidigitali kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kila siku; sheria ya utumishi wa umma, wajibu na haki za kila mfanyakazi na kujadili maslahi ya wafanyakazi; mahusiano mahala pa kazi; na nidhamu katika utendaji kazi.


Kikao hicho kimejumuisha Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo; Dkt. Jim Yonazi; Mameneja wa TPC wa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika hilo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.