MTANGAZAJI

MABORESHO VIWANGO VYA KODI TANZANIA

 

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa hufanya maboresho ya viwango vya kodi kila mwaka ili kuongeza wigo wa kukusanya kodi na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.

Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis  alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum, Stella Fiyao, aliyeuliza ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuondoa kodi kandamizi kwa wafanyabiashara na kuweka kodi Rafiki ili kumsaidia mfanyabiashara.

Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019/20, Serikali ilifuta tozo na ada 54 zilizotozwa na Wakala, Taasisi na Mamlaka mbalimbali za Serikali ambazo hazikuwa Rafiki.

“Napenda kuchukua fursa hii kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitozi kodi kandamizi na itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ikiwa ni pamoja na kuongeza vivutio na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wazawa na wawekezaji kutoka nje”, alieleza Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kupitia na kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Ufanyaji wa Biashara nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment) wenye lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.