MTANGAZAJI

UONGOZI WA WILAYA YA ILEMELA WATAKIWA KUHAKIKISHA MIUNDO MBINU YA HOSPITALI MPYA INAKAMILIKA

 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis  akitoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt. Severine Lalika (hayupo pichani), kuhakikisha Hospitali mpya ya Wilaya ya Ilemela iliyopo eneo la Kabusungu, inawekwa vifaa tiba, umeme na maji haraka ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi kwa ufanisi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kuhakikisha vifaa tiba, umeme na maji vinapatikana kwa haraka katika Hospitali mpya ya Wilaya hiyo iliyojengwa katika eneo la Kabusungu  ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi kwa ufanisi.

Amelitoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na mradi wa Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori kinachojengwa eneo la Nyamhongolo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Jijini Mwanza kwa ufadhili wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis ametoa maagizo hayo baada ya Uongozi wa Wilaya ya Ilemela kumweleza kuwa majengo muhimu ya hospitali hiyo yamekamilika lakini hospitali haijaanza kutoa huduma kikamilifu kutokana na kutopelekwa vifaa tiba pamoja na ukosefu wa umeme na maji katika eneo la mradi.

 “Serikali imetoa fedha nyingi kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Hospitali hiyo hivyo haiwezekani ikabaki bila maji na umeme kwa kuwa ni muhimu katika uendeshaji wa Hospitali, lakini nawapongeza kwa ujenzi madhubuti wa hospitali, majengo ni mazuri na imara”, alisema Mhe. Mwanaidi Ali Khamis

Aliwataka watumishi wa Hospitali hiyo ambayo imeanza kutoa baadhi ya huduma kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, uzalendo na kutunza vifaa na miundombinu iliyopo ili lengo la Serikali la kujenga hospitali hiyo na kuwapa wananchi huduma bora za afya liweze kutekelezwa kikamilifu.

Mchumi wa Manispaa ya Ilemela Bw. Mophen Mwakajonga, alisema kuwa majengo saba ya hospitali hiyo yaliyokamilika ni pamoja na jengo la wazazi, jengo la wagonjwa wa nje, utawala, maabara, mionzi na stoo ya dawa.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ambapo shilingi bilioni 1.7 zilitolewa na Serikali Kuu na shilingi milioni 176 zinatokana na mapato ya ndani ambazo zimetumika kufidia eneo la mradi na  kiasi cha shilingi milioni 304 zimetumika katika ujenzi wa ukuta wenye urefu kilomita 1.41 kuzunguka hospitali hiyo.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.