MTANGAZAJI

DKT. NDUGULILE USO KWA USO NA BARAZA LA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile akizungumza na
watendaji wa Tume ya TEHAMA wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo, Dar es Salaam.
Wa tatu kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Andrea Mathew

 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania, Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini humo.


Dkt.Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA – CCC akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Andrea Kundo Mathew kwa malengo yakukutana na bodi, menejimenti na wafanyakazi wa taasisi za Wizara yake ili waweze kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuweka mwelekeo wa utendaji kazi wenye matokeo chanya.


Amesema kuwa wananchi wana malalamiko kuhusu huduma wanazozipata hususani kwenye mitandao ya simu kuhusiana na mabando yao kuisha, kubadilishiwa gharama za matumizi ya mabando, kupunjwa  mabando yao na fedha wanazotuma kwa njia ya mtandao na haya yote yanahitaji majibu na kupatiwa matibabu.


“Hatutaki kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato,tutakwenda kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate taarifa ya malalamiko mangapi yamepokelewa, mangapi yamefanyiwa kazi, mangapi yameisha na kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua changamoto za wananchi,” amesisitiza Dkt. Ndugulile.

Ameongeza kuwa ni vema tuwepo mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za mawasiliano na bidhaa za TEHAMA na taarifa na siri zao kwa kuwa sekta hiyo inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi madukani na watumie lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia huduma na bidhaa za TEHAMA na kuwe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Baraza ili kutekeleza sheria ya TCRA iliyounda Baraza 

Waziri huyo ameitaka Tume ya Taifa ya TEHAMA kuishauri vizuri Wizara ili kufahamu mwenendo na mwelekeo wa wapi wanataka kupeleka TEHAMA ndani ya nchi na kutambua wataalamu wangapi wa TEHAMA, wataalamu wa namna gani na watibu changamoto za aina gani katika sekta hiyo.


Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary Shao Msuya amesema kuwa Baraza limejipanga kushughulikia maelekezo yaliyotolewa kwa kuwa watumiaji wa huduma na bidhaa za TEHAMA wameongezeka tofauti na mwaka 2003 wakati Baraza linaanzishwa ambapo kulikuwa na huduma chache ya kupiga na kupokea simu na za vifurushi tu wakati hivi sasa kuna huduma za kutuma na kupokea pesa, tutaongeza kasi ya utendaji kazi ili twende na kasi ya ukuaji wa TEHAMA nchini.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA amesema kuwa watazingatia suala la usajili wa wataalamu wa TEHAMA pamoja na maeneo yao ya ubobezi ikiwemo usalama wa mtandao; utengenezaji wa programu; uchakataji na uhifadhi wa taarifa na data; na ubunifu ili nchi hiyo iwe na wataalamu wa kutosha na kuendana na mahitaji kwa kuzingatia kasi ya ukuaji wa TEHAMA duniani.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.