WADAU MKOA WA MARA WAKEMEA UKEKETAJI NA MIMBA ZA UTOTONI
Mkuu wa Wilaya ya Butiama Anna Rose Nyamubi akizungumza na
wajumbe wa Kamati ya ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto kwa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama
wakati akifungua mafunzo kwa kamati hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara Anna Rose Nyamubi amekema vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji na mimba za utotoni vinavyokatisha ndoto za watoto hasa wa kike za kuendelezwa katika kupata elimu.
Akifungua Mafunzo kwa Kamati ya ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ya Halmashauri ya Wilaya hiyo yaliyofanyika hivi karibuni amesema Wilaya ya Butiama imejipanga katika kuhakikisha inapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao kwa kushirikiana na wajamii husika wakiwemo wazee wa mila, watu mashuhuri na viongozi wa dini ili kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinatokomezwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Butiama Jumanne Sagini anasema nguvu ya viongozi wa kisiasa inahitajika katika kuhakiksha wanahusika katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili.
“Sisi viongozi wa siasa tuwajibike kwa nafasi zetu tuoaze sauti kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya wananwake na watoto kwani inawezekana tukiamua kwa pamoja” alisema
Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT Butiama Joseph Mgabu amesema kuwa viongozi wa dini wana jukumu kubwa sana katika mapambano dhidi ya vitendo vya kikatili hasa katika kutoa elimu kwa waumini wao katika nyumba za ibada kwani itasaidia jamii kujua madhara ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake Hesha Kisibo ameiomba jamii kuachana na mfumo dume unaowakandamiza na kuwanyimwa wasichana na wanawake haki zao hivyo kusababisha kutokea kwa vitendo vya kikatili.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Grace Mwanga akitoa taarifa kwenye mafunzo hayo ameeleza kuwa jumla ya Kamati za Ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto 16343 zimeanzishwa katika mikoa Halmashauri, Kata na Vijiji ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.
Grace amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imeweza kuratibu mafunzo kwa Kamati hizo kwa kushirikiana na Shirika la UNFPA ili kuzipa nguvu Kamati hizo katika kutekeleza majukumu yake.
Ameongeza kuwa Wizara inatekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) unaolenga kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili kwa asilimia hamsini nchini.
Post a Comment