MTANGAZAJI

HUAWEI TANZANIA YATOA MAFUNZO YA TEKNOLOJIA YA 5G

 Huawei

Watanzania 24 wamehitimu mafunzo ya Teknolojia mpya ya 5G na teknolojia mpya ya 5G yaliyotolewa na Kampuni ya simu ya Huawei Tanzania na kutunukiwa vyeti na  Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainabu Chaula  katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano uliopo Mji wa Serikali, Mtumba mkoani Dodoma.


Wahitimu wa mafunzo hayo ni wataalamu watano 5 kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), wataalamu 8 kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wataalamu 10 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na mtaalamu mmoja kutoka Tume ya Taifa ya TEHAMA.


Dkt. Zainabu Chaula amewapongeza wahitimu kwa kumaliza mafunzo hayo ambayoyamefanyika nje ya muda wa kazi na kuwashukuru Huawei Tanzania kwa ushirikiano wao endelevu na kuwawezesha watumishi wa Sekta ya Mawasiliano pamoja na taasisi zake kuifahamu teknolojia mpya ya 5G.

Naye Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Mhandisi Aweso Aweso ambaye ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo amesema kuwa, teknolojia mpya inapotambulishwa ni jukumu la wataalamu wa Serikali kujifunza na kuielewa ili kuwawezesha katika kutunga Sera, ambazo zitasaidia kusimamia mwenendo mzima wa miundombinu ya TEHAMA na matumizi ya huduma za mawasiliano.


Aliongeza kuwa teknolojia ya 5G ni teknolojia yenye sifa za ziada kwa sababu ina akisi akili za binadamu, hivyo itasaidia Serikali kutoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi wake kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye kasi.


Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huawei Tanzania, Damon Zhang amesema Tanzania imeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya TEHAMA kwa kuhakikisha kila kona ya nchi imefikiwa na miundombinu hiyo, hivyo nchi kuweza kuleta mabadiliko ya kweli na kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda.


Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya TEHAMA amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye viwango bora zaidi, na mafunzo yaliyotolewa na kampuni ya Huawei Tanzania ni hatua nzuri ya kuwajengea uwezo wataalamu ili kuleta ushindani na mataifa mengine.


Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Mulembwa Munaku amesema kuwa mafunzo hayo ya teknolojia ya 5G ambayo yametolewa na Kampuni ya Huawei Tanzania kwa wataalamu wazalendo watanzania ambapo yamejikita katika masuala yanayohusu teknolojia mpya ya 5G katika usimikaji wa miundombinu, usambazaji wa huduma za mtandao, mahitaji ya mpangilio na mgawanyo wa masafa, mpango wa biashara na usimamizi wa
teknolojia mpya ya 5G.


Munaku ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya teknolojia mpya ya 5G kwa wataalamu wengine wa Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na teknolojia mpya.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.