MTANGAZAJI

SEKTA TA FEDHA NCHINI TANZANIA YATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga (katikati), akizindua Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2020 hadi 2030, kushoto ni Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara hiyo, Dkt. Charles Mwamwaja na kulia ni Mkurugenzi Idara ya Sera za Kodi, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Khamis Shibu Mwalim, katika ukumbi wa Wizara hiyo jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2020 hadi 2030, jijini Dodoma.

 Sekta ya Fedha nchini Tanzania imetakiwa  kuongeza ubunifu ili kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo na zitakazojitokeza katika sekta hiyo muhimu ambayo inamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James, katika uzinduzi wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (Fianancial Sector Development Master plan) kwa mwaka 2020 hadi 2030.


Aliainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo, ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma za fedha ambapo ni asilimia 8.6 tu ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki ikilinganishwa na asilimia 32.1 kwa wale wanaoishi mijini.


Amesema  kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Wasimamizi na Waratibu wa Sekta ya Fedha kutakiwa kuwianisha mipango yao ili kuendana na Mpango huo uliozinduliwa ni pamoja na sekta zote ndogo zilizomo ndani ya Sekta ya Fedha kama benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya hifadhi ya jamii na Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha.

 

Ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imeandaa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/2021 – 2029/2030, ili utumike kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo kwa kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kulinda watumiaji wa huduma za fedha na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

 

 Mpango huo pia umeandaliwa ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya Sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo katika sekta hiyo.


Naye Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja, alisema maendeleo ya Sekta ya Fedha ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini na kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imefanya mageuzi kadhaa tangu miaka ya 1990 ili kuendeleza mfumo wa fedha wa uhakika unaozingatia soko kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Maboresho hayo yanajumuisha Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Maboresho ya Sekta ya Fedha ambayo yalilenga kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya fedha na kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha.

Kwa upande wa wadau walioshiriki katika uzinduzi huo wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa Mpango huo ambao wanaamini utachakia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa nchi kwa ujumla.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.