MTANGAZAJI

KILIMANJARO WAPONGEZWA KWA KUZINDUA MWONGOZO WA UWEKEZAJI

Mkoa wa Kilimanjaro, umepongezwa kwa kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kutaka kila mkoa ubainishe fursa za uwekezaji zilizopo na kuandaa mwongozo wa uwekezaji.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Joseph Kakunda katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Kilimanjaro uliondaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Akimwakilisha Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Selemani Jafo, Naibu Waziri huyo alisema kwamba agizo la Rais ambalo limelenga kuweka mikakati mahsusi ya kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Akitoa salamu za pongezi kwa Mkuu wa mkoa, Mh. Anna Mghwira Naibu Waziri Kakunda alisema wakati mkoa wa Kilimanjaro unatekeleza maagizo, serikali kuu nayo inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuvutia wawekezaji mbalimbali.

Akizungumzia Mwongozo huo Naibu Waziri alisema kwamba kazi ya kubaini fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali yenye faida siyo tu kwa wawekezaji pekee bali pia kwa taifa letu kupitia kodi na upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa kila eneo la nchi.
Alisema kazi iliyofanywa na mkoa huo ina maana kubwa kwa kuwa sasa inakuwa rahisi kwa wawekezaji wawe wa ndani au nje kujua namna ya kuwekeza katika mkoa wa Kilimnjaro kwa kuzingatia mahitaji yao na namna rasilimali watu na miundombinu ilivyo.
Alisema agizo la Rais la utengenezaji wa mwongozo unakwenda sanjari na ubainishaji na uandazi wa maeneo ya uwekezaji ili yanapotakiwa yapatikane hima.

Aliutaka mkoa huo kuutangaza mwongozo wao kwani biashara ni matangazo katika maeneo mbalimbali ya kimataifa na ya wawekezaji katika masoko ya hisa kwa njia ya kielektroniki ili wavune utayari wao wa kukaribisha uwekezaji.
Kakunda alisema kwamba mkoa huo kwa asili unaweza kabisa kuvutia wawekezaji. Kinachostahili kufanywa kwa sasa ni kuhakikisha kauli mbiu ya Kilimanjaro ya Viwanda, inawezekana chukua hatua inatekelezwa kwa vitendo.

Akizungumza kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira alisema kwamba Mwongozo huo utafanyiwa kazi na matunda yake yataonekana wakati taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Alisema mkoa huo una rasilimali za kutosha kuwezesha wawekezaji mbalimbali kutekeleza adhma ya kuwa na viwanda vidogo na vya kati vinavyotumia rasilimali kutoka mkoani.

Aliwashukuru wataalam wa ESRF waliwezesha kupatikana kwa muongozo huo na wafadhili ambao ni UNDP.

Naye Dk Tausi Mbaga Kida, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) ambayo ndiyo ilipewa jukumu na Mkoa wa Kilimanjaro kufanya utafiti na uchambuzi wa kina ili kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa, aliupongeza mkoa wa Kilimanjaro kwa kuona umuhimu wa kuwa na mwongozo wa uwekezaji.

Aidha katika hotuba yake hiyo alisema kuwa taasisi yake ilitengeneza sehemu tatu za taarifa ambazo zote zililenga kutoa uwanda mpana kwa wawekezaji kuwa na taarifa muhimu za uwekezaji katika mkoa wa Kilimanjaro.

Mapema mwaka huu Mwongozo kama huo ulizinduliwa Mkoani Simiyu ambao umeleta matokeo makubwa ndani ya muda mfupi. Wiki mbili zilizopita mkoa wa Mwanza nao ulizindua mwongozo wa uwekezaji. Mkoa wa Mara katika siku za usoni unatarajiwa kuzindua mwongozo wa uwekezaji. Miongozo yote hiyo imeandaliwa na ESRF. 

Alisema miongozo hiyo ya Uwekezaji inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 – 2021) unaosisitiza ujenzi wa Tanzania ya Viwanda ili kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025.

   
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Joseph Kakunda (wa nne kulia), Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (wa tatu kushoto), Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira (wa nne kushoto), Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Aisha S. Amour (wa tatu kulia) Mkuu wa Idara ya Maarifa na Ubunifu wa ESRF Bi. Margareth Nzuki (wa pili kulia), Mtafiti Mshiriki wa ESRF, Dkt. Hoseana Lunogelo (kulia), Watafiti vijana kutoka ESRF Bw. Mussa Martine (kushoto) pamoja na Bw. Joseph Nyampepela Ngonyani (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja huku wakiwa wameshika nakala za Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kilimanjaro.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.