MTANGAZAJI

HISPANIA YASAIDIA SHILINGI BILIONI 3.1 KUKABILI UMASKINI TANZANIA

IMG_0820
Balozi wa Hispania nchini Tanzania, Mh. Luis Cuesta Civis (kulia) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez (katikati) wakiwasili kwenye ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kabla ya ziara ya kuelekea katika kijiji cha Chasimba kukagua miradi inayofadhiliwa na TASAF katika wilaya ya Bagamoyo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga.(Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog).

Na Modewjiblog , Bagamoyo
Serikali ya Hispania imetoa shilingi bilioni 3.1 kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii nchini Tanzania ambayo mingine inatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF. 
 
Fedha hizo zimetolewa kupitia mfuko wa maendeleo endelevu (SDGF) zilizotolewa kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya shughuli zake hapa nchini.
 
Mashirika hayo ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ,Shirika la Umoja wa Mataifa la watoto (UNICEF) , Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA), na Shirika la Kazi Duniani( ILO).
 
Hayo yamesemwa katika ziara ya Balozi wa Hispania nchini, Luis Cuesta Civis na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez katika kijiji cha Chasimba kilichopo wilayani Bagamoyo, Pwani jana.
 
Ziara yao ilikuwa ya kukagua miradi inayofadhiliwa na TASAF katika wilaya ya Bagamoyo. Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya nane zilianza kupokea fedha za TASAF na kuonekana kuleta mabadiliko makubwa katika jamii. 
 
Hata hivyo moja ya shughuli wanazofanya wakazi wa Chasimba ni kilimo wakiwa na pato la sh 350,000 kwa mwaka.
 
Huduma za jamii zinazopatikana katika vijiji hivyo ni pamoja na shule ya msingi, barabara inayopita kijiji ni hapo na zahanati. 
 
Wakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya TASAF jamii ya Chasimba ilijenga madarasa matatu na ofisi ya walimu. Miradi hiyo ilizinduliwa mwaka 2007 na kukamilika mwaka 2008. Katika miradi hiyo TASAF ilichangia 30,415,471. 
 
Aidha kijiji cha Chasimba ni miongoni mwa vijiji 17 ambavyo vinatekeleza mradi wa CB-CCT toka mwaka 2008/2009. Katika kipindi hicho wamepata ruzuku ya jumla ya sh 28,325,400. 
 
Pia kijiji hicho kina kaya 197 zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III (PSSN) ambapo tayari wamepewa ruzuku ya shilingi 43,227,190 katika mikupuo 9. 
 
Akizungumza kijijini hapo Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez aliishukuru serikali ya Tanzania na Hispania kwa kufanikisha shughuli hiyo nzito ya kusaidia jamii kukabiliana na umaskini.

IMG_0803
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (kulia) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez wakisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo.
Tunashukuru serikali ya Tanzania na Hispania kwa kushirikiana kusaidia wananchi wa Tanzania kukabiliana na umaskini. Kwa kufanyakazi na watu wa hali ya chini kabisa miradi hii imewezesha familia kupeleka shule watoto wao, kushiriki katika mipango ya uwekaji wa akiba na kuongeza kipato. Jukumu letu la pamoja ni kuondoa umaskini Tanzania” alisema Alvaro.

Naye Balozi wa Hispania Luis amesema kwamba serikali ya Hispania inaamini katika kusaidia kupambana na umaskini kwa kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazowakabili. 

Alisema wataendelea kufanya hivyo kupitia Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo yanafanyakazi kwa kushirikiana na serikali za mikoa na mitaa ambazo ndizo ziliopo karibu na wananchi husika.

 Alisema kwamba wanaamini mradi wa kunusuru kaya maskini unafanya wajibu wake kwa kuwafikia wananchi maskini sana.Alisema mradi huo ni moja ya miradi inayoonesha umuhimu wa kufanyakazi pamoja kati ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa na nchi wahisani.Kijiji cha Chasimba pia kinafanya kazi za ujenzi mbalimbali kuanzia Machi 23, mwaka jana. 

Kazi hizo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kilomita 1.1 ya Chasimba-Kiegea.Aidha kumekuwepo na mafanikio makubwa tangu kuanza kwa mradi wa PSSN kijijini hapo.Alisema kumekuwepo na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa na kuhudhuria shule, aidha madarasa matatu yamejengwa na ofisi ya mwalimu. 

Akizungumzia mafanikio Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga alisema kuna mabadiliko makubwa katika maisha ya watu kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo katika kijiji.Aidha wananchi wa Chasimba wamepata ushawishi mkubwa wa kushiriki katika miradi ya maendeleo ndio sababu ya mafanikio yanayoonekana. 

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mradi wa kunusuru kaya maskini umesaidia watoto kwenda shuleniwakiwa wametimiziwa mahitaji yao yote. Aidha mradi huo umeweza kufanikiwa kufanya watu wapendekwenda kiliniki na kuangalia afya za mama na watoto.

 Aidha familia zilizopewa fedha sasa wamebadilisha namna ya mfumo wa kupata lishe na kuwa na uhakika na lishe. 

Aidha ujira kutokana na kazi unaotarajiwa kutolewa ni jumla ya dola za Marekani 15,991 wakati gharama za vifaa na ufundi ni dola za Marekani 5,328.Jumla ya kaya 197 zitashiriki katika miradi ya ujenzi kwa kipindi cha miezi minne na utaendelea kwa miaka miwili katika kipindi hicho hicho.
IMG_0824
Balozi wa Hispania  nchini Tanzania, Mh. Luis Cuesta Civis (kulia), Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahali (katikati) wakielekea kwenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kupokea taarifa ya mradi wa TASAF katika wilaya ya Bagamoyo.
IMG_0838
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahali (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwenye mkutano wa kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi ya TASAF katika wilaya ya Bagamoyo kwa wadau wa maendeleo waliotembelea wilaya hiyo kukagua miradi inayofadhiliwa na Tasaf. Kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez sambamba na Balozi wa Hispania nchini Tanzania, Mh. Luis Cuesta Civis (wa pili kulia) na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Bagamoyo, Hilda Gadi.
IMG_0854
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga akizungumza kwenye mkutano mfupi wa kupokea taarifa ya miradi inayofadhiliwa na TASAF wilayani Bagamoyo. Wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Bi. Hilda Gadi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahali (katikati), Balozi wa Hispania nchini Tanzania, Mh. Luis Cuesta Civis (wa pili kulia) pamoja na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez.
IMG_0873
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Bi. Hilda Gadi akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa TASAF wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika wilaya ya Bagamoyo mbele ya wadau wa maendeleo.
IMG_0894
Balozi wa Hispania nchini Tanzania , Mh. Luis Cuesta Civis akizungumzia ufadhili wa serikali yake kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii nchini ambayo mingine inatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF.
IMG_0924
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez akizungumza katika mkutano huo ambapo aliishukuru serikali ya Tanzania na Hispania kwa kufanikisha shughuli ya kusaidia jamii kukabiliana na umaskini ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Malengo ya Millenia (MDG's).
IMG_0855
Baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa TASAF wakishiriki kwenye mkutano huo.
IMG_0861
IMG_0860
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo.
IMG_0948
Picha ya pamoja mara baada ya mkutano.
IMG_0954
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (katikati) akijadiliana jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez (kulia) pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahali (kushoto).
IMG_0967
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Bi. Hilda Gadi. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, John Mahali.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.