MTANGAZAJI

MARA:MTOTO AFARIKI BAADA YA KUUNGULIA NDANI YA NYUMBA ALIMOKUWA AMELALA


Mtoto mwenye umri wa miaka mitano Mkami Chacha Kandy amefariki dunia kwa kuungulia ndani  ya nyumba aliyokuwa amelala baada ya nyumba hiyo kuunguzwa na moto uliosababishwa na mshumaa katika kitongoji cha Mwisori,  kijiji cha Kinesi, kata ya Nyamunga, Tarafa ya Nyancha, Wilayani Rorya.

Tukio hilo lilitokea juni 30 majira ya saa tatu usiku ikidaiwa kuwa chanzo cha nyumba kuteketea ni moto wa mshumaa uliokuwa ukitumika kuwaangazia watoto wanne wakati wa kuandaa malazi kisha kuuacha mshumaa huo ukiwaka  na watoto watatu kwenda kutazama luninga kwenye nyumba nyingine wanamolala wazazi wao ndipo mshumaa  uliangukia kwenye godoro alilokuwa amelala marehemu na nyumba yote kuunguzwa na moto.

Mwandishi wa Morning Star Radio amesema kuwa wazazi wa Marehemu wana nyumba nne na watoto wanne pamoja na marehemu walikuwa wakilala kwenye nyumba yao na huenda hali ya ulemavu wa Mkami Chacha ilisababisha ashindwe kupiga kelele na kujiokoa.

Chacha Dominiko mzazi wa Mkami Chacha Kandy amesema kuwa wakati nyumba ya watoto inawaka moto wao walikuwa wanangalia maigizo kwenye luninga ya nyumba yao nyingine wanamolala.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwisori Patrick Peter alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa yeye alikuwa mmoja wa wale waliokuwa wa kwanza kufika kwenye tukio lakini walishindwa kumwokoa mtoto huyo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.