MTANGAZAJI

MARA:HEKTA 526 ZA ZAO LA MAHINDI ZAATHIRIWA NA UGONJWA WA MLND



Jumla ya hekta 526 za zao la mahindi zimeathirika  na ugonjwa wa “Maize Lethal Necrosis ” ambao umeshambulia mazao hayo katika kata 16 kati ya 24 wilayani Tarime.

Sylivester Gwiboha ambaye ni  afisa kilimo chakula na umwagiliaji wa  Wilaya ya Tarime amesema kata zilizoathiriwa kwa kiwango cha hekta ni Kibasuka 51, Nyarukoba 85, Gorong’a 120,Kemambo 12, Nyanungu  45, Itiryo 23, Muriba 29, Nyansincha 7, Nyamwaga 55, Pemba 15,Nyakonga 5, Mbogi 35, Binagi 11,Komaswa 5, Nyarero 10 na kata ya Manga 8.

Idara inawataka wakulima kuepuka kununua mbegu za mahindi nje ya maduka ya pembejeo yaliyosajiliwa ili kuepuka kuingiza mbegu zenye virusi hatarishi.

Gwiboha amesema watakuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka yanayouza mbegu za mahindi kiholela na atakayebainika kuuza mbegu zisizo kubarika atafikishwa mahakamani.

 Wakulima wameshauriwa wasirudie rudie kulima zao moja kwenye shamba moja kwa zaidi ya msimu mmoja mahindi yaliyoshambuliwa shambani yang’olewe mara tu yanapobainika na kuchomwa moto kabla hayajaeneza ugonjwa shamba zima.

 Ugonjwa huo kwa mara ya kwanza nchini Tanzania uliripotiwa kuonekana mwaka 2012 katika mikoa ya Mwanza,Mara, Arusha, Manyara na Moshi na nchini Kenya mwaka 2011 katika eneo la Longisa na Bomet chini.

Wilaya ya Tarime ina wakazi 393,693 ambao kwa mwezi hutumia  tani 8981.12 za mahindi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.