DAR ES SALAAM:WAWILI WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA UJAMBAZI
Watu wawili wamekamtwa kwa tuhuma za mauaji ya Sista
Clesencia Kapuli (50) wa Kanisa Katoliki,
aliyekuwa Mhasibu katika Shule ya Sekondari Mwenyeheri, jijini Dar es
Salaam.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
limesema watu hao ni kati ya watu wanane waliokamatwa kwa tuhuma za ujambazi
sugu wa kutumia silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman
Kova, amesema watu hao walikamatwa juzi
katika operesheni iliyofanywa na jeshi hilo kwa kutumia vikosi maalum.
Amesema licha ya watu hao wawili kuhusika katika
tukio la mauaji ya sista huyo, lakini pia walihusika katika tukio la kupora
fedha katika benki ya Barclays tawi la Kinondoni miezi michache iliyopita.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ni Manase Ogenyeka
(35), mkazi wa Tabata na Hamis Ismail, mfanyabiashara na mkazi wa Magomeni
Mwembechai.
Pia Jeshi la Polisi limesema linaendelea na
operesheni hiyo pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika katika
tukio la maujai ya sista Kapuli, Juni 23,
mwaka huu, pamoja na mmoja aliyehusika katika tukio la wizi wa fedha katika
benki ya Barclays.
Sista huyo ambaye
alikuwa mhasibu wa Shule ya Sekondari Mwenyeheri iliyopo Makoka wilayani
Kinondoni, aliuawa Juni 23, mwaka huu
kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa
katika pikipiki aina ya Boxer.
Post a Comment