MTANGAZAJI

IDADI YA WATANZANIA YAFIKIA MILIONI 48



Idadi ya Watanzania  imeongezeka kutoka milioni 44.9 baada ya miaka miwili ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012  hadi kufikia milioni 48 mwaka huu

Hayo yalibainishwa  na Rais wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete wakati akizindua chapisho la tatu la taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi na matumizi ya tovuti katika kupata taarifa mbalimbali za sensa na makazi ya watu linalotokana na sensa ya watu na makazi ya 2012.

Akizindua chapisho hilo jana, Rais Kikwete alisema kumekuwapo na kasi ya ongezeko la watu nchini na kwamba hadi sasa jumla ya idadi ya watu nchini imefikia milioni 48 kutoka milioni 44.9 baada ya kukamilika kwa zoezi la sensa ya watu na makazi  mwaka juzi.

Kwa mujibu wa Kikwete, kutokana na kasi hiyo ya kuongezeka, mwaka 2016 idadi ya Watanzania inatarajia kufikia milioni 50, mwaka 2025 milioni 63 na mwaka 2050 ikifikia milioni 125.

Matokeo ya sensa hiyo katika chapisho hilo pia yanaonyesha asilimia 33 sawa na idadi ya wanawake milioni 9.2 nchini ndiyo wanaotunza kaya zao kutokana na  sababu za umaskini wa kipato.

Pia matokeo ya chapisho hilo yanaonyesha kuwa wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 50 mwaka 1988 hadi kufikia miaka 61 mwaka 2012 kutokana na kwamba kwa wale wenye  umri wa miaka zaidi ya 61 wana uwezo wa kuishi miaka 18 zaidi kutokana na jitihada za serikali za kuboresha huduma za afya nchini.

Mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Dk. Albina Chuwa, amesema chapisho hilo linaonyesha kupungua kwa kiwango cha uzazi nchini kutoka wastani wa watoto 6.5 mwaka 1988 hadi wastani wa watoto 5.2 mwaka 2012.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.