MTANGAZAJI

WHO YAAGIZA VIPIMO KWA AJILI YA KUPAMBANA NA UGONJWA WA DENGUE NCHINI TANZANIAShirika la Afya Duniani (WHO), limejiunga katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuagiza vipimo 1,000 kwa ajili ya upimaji nchi nzima.

WHO imechukua hatua hiyo kusaidia juhudi zinazoendelea za kupambana na homa hiyo na imeagiza utafiti zaidi ufanyike ili kutambua aina halisi ya virusi vya dengue vilivyopo nchini kwa kulinganisha na vile vinavyopatikana katika maeneo mengine duniani.

Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa WHO, Dk Grace Saguti amekaririwa na vyombo vya habari nchini Tanzania jana ambapo amesema tayari chombo hicho kimeagiza vipimo hivyo vitakavyogharimu takribani shilingi milioni 18 na kila kimoja kinaweza kupima sampuli 25, hivyo kunufaisha watu 25,000.

Hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya hospitali za Serikali za wilaya na rufaa zinakabiliwa na uhaba wa vipimo, hali iliyosababisha kutoza kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 kwa ajili ya kupima mgonjwa mmoja.

Gazeti moja la kila siku nchini Tanzania jana liliandika habari inayoeleza kuwa katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.

Juhudi hizo za WHO zimetangazwa siku moja baada ya Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe kulieleza Bunge kuwa kwa sasa vipo vipimo 350 na Serikali inatarajia kuagiza vingine 750.


Hadi jana takwimu za Serikali zinaonesha kuwa idadi ya watu waliougua ugonjwa wa dengue nchini Tanzania wamefikia 460.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.