MTANGAZAJI

ASILIMIA 36 YA WANAOTUMIA DAWA ZA KULEVYA TANZANIA WANA MAAMBUKIZI YA VVU



Asilimia 36 ya watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya
kujidunga sindano nchini Tanzania, wana maambukizo ya VVU.takwimu hizo huenda zikaongezeka, ikiwa jamii haitaelimishwa jinsi ya kupunguza madhara dhidi ya dawa hizo.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Sa-laam hivi karibuni na Mratibu wa Mtandao wa watu wanaotumia Dawa za kulevya (TannPuD), Happy Assen kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara kwa watumia dawa za kulevya.

Amesema ingawa matumizi ya dawa za kulevya ni makubwa nchini, bado jamii haiko karibu na watu wanaotumia dawa hizo, na badala wametengwa kama wahalifu, na kusahau kwamba nao pia ni sehemu ya jamii na wanapaswa kusaidiwa.

Amesema takwimu za afya na matumizi ya dawa za kulevya nchini, zinaonesha asilimia 36 ya watumia dawa za kulevya nchini kwa njia ya kujidunga sindano, wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Amesema hiyo inatokana na watumia dawa hizo, kuchangia bomba moja la sindano watu wengi wakati wa kujidunga dawa za kulevya aina ya heroine, kwa sababu hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua kila mmoja bomba lake.

Takwimu za hivi karibuni nchini Tanzania za matumizi ya dawa za kulevya, zinaonesha kwamba watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano ni 25,000, na kati ya hao 18,000 wapo Dar es Salaam.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.