MTANGAZAJI

KAMATI KUU TENDAJI YA WAADVENTISTA ULIMWENGUNI YATOA MAAMUZI


Kamati Kuu Tendaji (EXCOM) ya Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni (GC) imefanya Mkutano wa majira ya kuchipua  mwaka huu, Aprili 14 hadi 15 katika makao makuu yake Silver Spring, Maryland, Marekani. 

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa kanisa kutoka duniani kote, wakiwemo wajumbe wa Kamati Tendaji (EXCOM), maafisa wa divisheni na wenyeviti wa unioni, na ulifanyika kwa mfumo wa mseto, baadhi wakihudhuria ana kwa ana na wengine kwa kwa njia ya mtandao na ulirushwa kupitia Youtube.

Katika mkutano huo, masuala makuu yalikuwa ripoti za kifedha zilizokaguliwa, maamuzi ya kiutawala na mikakati ya kuendeleza utume wa kanisa hilo duniani, sambamba na kuangazia nafasi ya teknolojia katika uratibu wa kazi za kimataifa.

Ripoti ya hazina ilionyesha kuwa licha ya changamoto za uchumi duniani kama mfumuko wa bei, migogoro na mabadiliko ya thamani ya sarafu, kanisa lilifunga mwaka 2025 likiwa na ziada ya fedha. Mali zilifikia dola za kimarekani milioni 677, mali halisi zikiongezeka kwa dola milioni 32.7, huku faida ya uendeshaji ikiwa dola milioni 25. Mapato ya uwekezaji yalifikia dola milioni 27 na Zaka zikabaki karibu dola milioni 89. Matumizi yalifikia dola milioni 281, ambapo asilimia 80 ilielekezwa kwenye shughuli za utume.

Mweka Hazina Msaidizi Timothy Aka alionya kuhusu hatari zinazoendelea ikiwemo kupanda kwa gharama za mafuta, mfumuko wa bei na hali ya kisiasa duniani. Aliyewahi kuwa Kiongozi wa kanisa hilo duniani  Jan Paulsen aliibua hoja kuhusu maadili ya uwekezaji, huku Mweka Hazina Mkuu Paul Douglas akieleza kuwa kanisa hutumia kamati ya ndani na miongozo maalum kusimamia uwekezaji huo. Viongozi wastaafu  G. T. Ng na Ted N. C. Wilson waliisifu ripoti hiyo, wakieleza kuwa usimamizi mzuri umechangia kupatikana kwa ziada hiyo.

Katika hatua nyingine, mkutano huo uliidhinisha kuunganishwa kwa Unioni Konferensi za Kaskazini na Kusini mwa Ujerumani kuwa Union Konferensi ya Ujerumani ifikapo mwaka 2027. Makamu wa Mwenyekiti wa GC, Thomas Lemon alisema hatua hiyo inalenga kurahisisha uongozi na kuimarisha utume, huku Katibu Msaidizi Karen Porter akieleza kuwa itasaidia kuboresha matumizi ya rasilimali na kukabiliana na mabadiliko ya kijamii.

Aidha, Kamati Tendaji imethibitisha tarehe za Mkutano Mkuu wa 63 wa GC utakaofanyika Juni 20 hadi 29 mwaka 2030 mjini Indianapolis, Indiana. Marekani. 

Kiongozi wa Kanisa hilo  Köhler alisema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto za usafiri, huku Mweka Hazina Msaidizi Sabrina D’Souza akikumbusha kuwa mkutano wa mwaka 2020 ulisitishwa kutokana na janga la Uviko-19. Pia ilielezwa kuwa mipango ya mkutano wa mwaka 2035 inaangaliwa, ikiwemo uwezekano wa kufanyika nje ya Marekani.

Katika hatua nyingine mkutano huo uliangazia mpango wa kimataifa wa uinjilisti wa OneVoice27 unaolenga kampeni ya pamoja  Septemba 2027. Uzinduzi wake umepangwa kufanyika Septemba 5, 2026. Mweka Hazina Msaidizi Richard Stephenson aliwasilisha ratiba ya utekelezaji, huku Katibu wa Wachungaji Ramon Canals akisisitiza umuhimu wa maombi na maandalizi ya kiroho.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Alyssa Truman alitambulisha kaulimbiu ya mpango huo, “Mambo Yote Mapya: Tumaini Linaanzia Hapa,” huku Mkurugenzi wa Kituo cha Utume Ulimwenguni, Chanmin Chung akisisitiza umuhimu wa kuelekeza juhudi katika miji mikubwa.

Kifedha, mpango huo umevuka lengo lake la awali la dola milioni 27 na kufikia dola milioni 42 kutoka divisheni mbalimbali. Mweka Hazina Msaidizi Gideon Mutero alisema rasilimali hizo zitasimamiwa kwa mfumo maalum ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi katika kutekeleza utume.

Akihitimisha mkutano huo, Katibu wa GC, Richard McEdward alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba ujumbe wa tumaini unahitajika zaidi, akitoa wito kwa waumini kushiriki kikamilifu katika utume wa kanisa.




No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.