MTANGAZAJI

WAFANYAKAZI WA MORNING STAR RADIO NA MORNING STAR TV WATAKIWA KUWA NA UMOJA

Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Mch Steven Bina amewataka wafanyakazi wa Morning Star Radio na Televisheni kuwa na umoja katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Steven Bina ambaye ni mmoja wa viongozi wa kanisa hilo aliyeshiriki kwenye mchakato wa uanzishwaji wa Morning Star Radio nchini Tanzania mwaka 2003 amesema umoja na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa Taasisi hizo ndiyo njia pekee ya kuleta mafanikio katika utendaji wa kazi wa vyombo hivyo vya habari vya kanisa.


Mchungaji Bina ambaye ndiye msimamizi wa vyombo vya habari vya Kanisa la Waadventista Wa Sabato katika kanda inayojumuisha nchi 11 pia amewataka viongozi wa taasisi hizo kushirikiana na wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu yao.


Kanisa la Waadventista Wa Sabato nchini Tanzania linamiliki kituo cha Morning Star Radio inayosikika katika mikoa 10 kwenye masafa ya fm,satalaiti na kwenye mtandao duniani kote, ambapo sasa liko katika maandalizi ya uanzishwa wa kituo cha televisheni ya Morning Star.


Kwa mujibu wa Mchungaji Steven Bina kuanzia mwaka 2006 Kanisa la Waadventista Wa Sabato katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lilikuwa na studio za kutayarisha vipindi vya radio vitatu ,vituo vya radio vya fm na televisheni vitatu,vituo 1000 vya satalaiti katika makanisa mahalia, ambapo kwa sasa kuna vituo vya radio za fm 30,studio 3,vituo vya televisheni 13.vituo vya satalaiti 6000 ambavyo hupokea matangazo kutoka kituo cha Hope Channel kinachomilikiwa na kanisa hilo duniani.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.