WANANCHI WA LUCHELELE MWANZA WATAKA MKUU WA KITUO CHA POLISI AONDOLEWE
Wakazi wa Luchelele,kata
ya Mkolani,wilayani Nyamagana,wamemtaka Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Valentino Mlowola
kumchukulia hatua kali za kinidhamu Mkuu wa kituo cha Polisi cha Igogo,kufuatia
kuachiwa huru watuhumiwa wa ujambazi,mauaji na ubakaji katika eneo hilo.
Wakizungumza jana katika
Mkutano wa wananchi hao na Kamanda wa Polisi Mwanza,uliofanyika katika Shule ya
Msingi Luchelele, wananchi hao wamesema hawana imani na Mkuu huyo wa kituo cha
polisi cha Igogo,kufuatia matukio mengi ya uhalifu kutokea kila mara eneo
hilo,bila watuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wamemtaka Mkuu huyo wa
Polisi Mkoani Mwanza kuwakamata upya watuhumiwa wa matukio ya ujambazi,ubakaji
na mauaji yaliyotokea Feburuari 7 mwaka huu eneo hilo,lakini watuhumiwa wawili
kati ya wanne wakaachiwa huru.
Ili kurejesha imani kati
ya wananchi hao na jeshi la polisi,wananchi hao walitaka jeshi la polisi
kufuatilia upya jalada la kesi hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoani
Mwanza,Valentino Mlowola,mapema wiki hii
aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa wawili kati ya wanne wa kesi
hiyo waliachwa huru na ofisi ya Wakili wa Serikali Mkuu Mfawidhi Mkoani
Mwanza,kulingana na taratibu na mfumo wa mwenendo wa makosa ya jinai.
Kamanda Mlowola
amekubali kufanyia kazi madai ya wakazi wa eneo hilo,ikiwemo kumhamisha Mkuu
huyo wa kituo cha Igogo,na kuwajengea kituo kipya cha polisi katika eneo la
Luchelele,ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara eneo hilo.
Na:Conges Mramba-Mwanza
Post a Comment