MTUHUMIWA WA UDUNGUAJI TARIME ALIVYONASWA HUKO TANGA
Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya Justus Kamgisha akionesha Waandishi wa habari (hawapo pichani) Bunduki iliyokuwa ikitumika kwa mauaji ya raia wasiokuwa na hatia Wilayani humo |
Mtuhumiwa wa mauaji ya watu tisa wilayani hapa, ametiwa mbaroni huku mwenzake akiuawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Polisi
Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya kwa kushirikiana na raia wema na Polisi
wa Mkoa wa Tanga ndio waliofanikisha ukamataji wa mtu huyo.
Mauaji
ya watu hao tisa yalianza kutekelezwa Januari 25-27 na mtu anayedaiwa
kuwa ni Charles Range Msongo au Josephat Chacha Kichune (38) mkazi wa
kijiji cha Kenyamanyori.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, mtu aliyeuawa alitambuliwa
kwa majina ya Marwa Keryoba (42) mkazi wa kijiji cha Kebeyo ambaye
inadaiwa alikuwa mhifadhi wa silaha iliyotumika kwa mauaji hayo.
Kamanda
Kamugisha alisema wakati Kichune akikamatwa Februari 6 mkoani Tanga,
Keryoba aliuawa mjini Musoma mkoani Mara katika majibizano ya kurushiana
risasi na polisi.
Alisema Kichune alikimbilia Tanga baada ya
msako mkali kuendeshwa mkoani Mara ukishirikisha polisi na raia wema,
ambapo ufuatiliaji wa Polisi ulibaini kuwa mtuhumiwa alitoroka kwa
pikipiki kutoka Kenyamanyori hadi Musoma.
Inadaiwa alipofika
Musoma alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Keryoba eneo la Nyabisare
kata ya Bweri na kuhifadhi bunduki aliyokuwa akiitumia kufanya mauaji..
“Baada
ya kuhifadhi silaha hiyo alipanda basi na kwenda Tanga akipitia Arusha
akitumia jina la Josephat Chacha kwenye tiketi yake … tulitoa taarifa
kwa askari wa Tanga ambao walifanikisha ukamataji ,” alisema Kamanda
Kamugisha.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa alipohojiwa na Polisi
alikiri kufanya mauaji ya watu wilayani Tarime hususan katika kata za
Turwa, Binagi na Kitare katika tarafa ya Inchage.
“Tulipomwuliza
alikohifadhi silaha akasema ameihifadhi kwa Keryoba ambaye alihamia
Bweri mwishoni mwa mwaka jana,” alisema na kuongeza kuwa walimchukua
mtuhumiwa akawaoneshe alikokuwa akiishi mshirika wake na walipofika
Keryoba alijaribu kutoroka akiwa na silaha.
“Alifyatua risasi
akiwaelekeza askari ambao walijibu mapigo na kumjeruhi lakini akafariki
dunia akiwa njiani kukimbizwa katika hospitali ya mkoa mjini Musoma …
tulichukua bunduki hiyo ya SMG iliyokatwa kitako, ikiwa na magazini
yenye risasi tisa huku moja ikiwa tayari imekokiwa,” alisema Kamanda.
Upekuzi
uliofanywa katika chumba alimokuwa akiishi Keryoba, ulibaini kuwamo
deki moja, tochi mbili, pea ya viatu vya buti, simu mbili za mkononi, CD
za picha mbalimbali, bidhaa za dukani na mpira wa baiskeli.
Polisi
ilipongeza wananchi hususan raia wema kwa kujitolea kutoa taarifa na
kuwaomba waendeleze moyo wa kushiriki mapambano dhidi ya uhalifu.
Alisema
Polisi itatoa zawadi ya Sh milioni moja kwa mtu atakayetoa taarifa
zitakazowezesha kukamatwa kwa silaha ya moto au watuhumiwa wa ujambazi.
Mtuhumiwa
huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote msako wa kukamata
watuhumiwa wengine wa tukio hilo utakapokamilika.
Hivi
karibuni, Kamanda Kamugisha alitangaza kukamatwa kwa watu 10 kutokana na
mauaji hayo huku akikataa kutaja majina yao akihofia kuvuruga upepelezi
na kusema mtuhumiwa inaonekana alikuwa akitumia silaha aina ya SMG au
SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa maeneo ya mauaji.
Mauaji
Januari
26, saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mogabiri, inadaiwa alimwua kwa
risasi Zakaria Marwa (28) na Erick Lucas (24) baada ya kukutana nao
njiani, kwa mujibu wa Polisi.
Siku hiyo hiyo
saa 4 usiku katika kijiji hicho alidaiwa kumwua Robert Kisiri (45) baada
ya kuvamia baa inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine.
Siku
iliyofuata saa 11.30 alfajiri inadaiwa alifanya mauaji mengine katika
kijiji hicho kwa kumpiga risasi David Matiko (39) na kumpora simu aina
ya Nokia.
Katika tukio hilo, alimjeruhi
Machungu Nyamahemba (19) ambaye alilazwa katika hospitali ya Tarime kwa
matibabu. Siku hiyo saa 2 usiku katika kijiji cha Nkende anadaiwa
kumwua Juma Nyaitara (30) na baada ya mauaji akapora simu za mkononi za
Chacha Magige na Masero Marigiri.
Chanzo:Samson Chacha wa Habarileo
Post a Comment