HALI YA USALAMA INATISHA WILAYA MPYA YA KAKONKO KIGOMA
Imenibidi nijitokeze hapa jukwaani kueleza hali ya usalama ilivyo
mbaya katika wilaya mpya ya Kakonko katika mkoa wa Kigoma. Wilaya hii ni
kati ya zile mpya zilizoanzishwa hivi karibuni. Mwanzoni ilikuwa ni
tarafa mojawapo za wilaya ya Kibondo.
Kijiografia, wilaya hii imepakana na wilaya ya Ngara, Kibondo pamoja na nchi ya Burundi.
Katika siku za nyuma, kati ya 1999-2003, hali yetu ya usalama
ilikuwa mbaya kiasi kwamba wananchi wengi waliibiwa mifugo, pesa na mali
zingine ikiwa ni pamoja na wengine kuuawa kwa risasi na mapanga! Hii
ilikuwa enzi za vita vya msituni vilivyompeleka madarakani Mhe. Rais
Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Baada ya kuona hali imekuwa tete, wananchi tuliendesha mikutano na
kupeleka maombi mkoani kuomba msaada wa ulinzi ambapo serikali
ilianzisha detach za JWTZ katika vijiji vingi vya mpakani vikiwemo vya
Rumashi, Gwarama, Muhange, n.k.
Hatimaye wananchi wakapata ahueni na kuendelea na shughuli za kujitafutia riziki.
Kwa masikitiko makubwa, hivi karibuni serikali iliamua kufunga
detach zake zote za vijijini na askari wote kurudishwa Kakonko! Hii
imepelekea kuibuka kwa unyama na ujambazi wa kutisha sana katika vijiji
vya wilaya hii.
Kwasasa watu hawalali, wanashindwa kufanya shughuli za uzalishaji
kwa kuhofia usalama wao. Ikumbukwe kuwa nchi ya Burundi imetoka vitani
na kuna vijana wengi walikuwa waasi na sasa wamerudi vijijini baada ya
jeshi la Taifa kuundwa upya! Vijana hawa wengi wao wanamiliki silaha na
wanazitumia kufanya uhalifu ndani ya Burundi na vijiji jirani vya
Tanzania.!!!
Labda niwape takwimu za utekaji wa magari na watu katika wiki mbili tu zilizopita:
Tar 22.10.2012, magari matatu yaliyokuwa yanatoka katika vijiji vya
Nyabibuye na Rumashi kuelekea Kakonko yalirushiwa risasi mfululizo
katika eneo la Muruhuru ambapo magari mawili yalifanikiwa kukimbia huku
moja likitekwa na abiria wote kupigwa na kunyanganywa kila kitu
walichokuwa nacho!
Tar 25.10.2012 , gari moja na pikipiki mbili zilitekwa katika eneo
la Kumkambati (katikati ya Rumashi na Nyabibuye). Abiria waliibiwa kila
kitu zikiwemo simu na pesa.
Tar 26.10.2012, magari matatu yalitekwa katika eneo la Ntanga (upande wa Ngara) ambapo abiria waliibiwa na kupigwa!
Jana tar 29.10.2012,magari mawili yametekwa eneo la Katengera yakielekea Kakonko!!
Na haya ni miongoni tu mwa matukio yanayotokea katika wilaya hii.
Sasa imekuwa ni hofu tupu kwa wananchi,kila mtu anaogopa hata kwenda shambani kulima hasa ukizingatia msimu huu ni wa kilimo.
Wafanya biashara wanazidi kukatwa mitaji na majambazi na wahuni
hawa! Wafanyakazi wanaogopa kufuata mishahara benki. Sasa wameanza
kuvamia nyumba za wafanya biashara usiku na kuwapora kila
wanachokikuta!!
Mimi kama mzaliwa wa eneo hilo (ninaishi Dsm),hali hii imenitisha
na kunihuzunisha sana. Watu wanazidi kudidimizwa kiuchumi na kuendelea
kuwa masikini.
Vile vile ni muhimu kukumbuka kuwa, katika vijiji kama vya Rumashi,
Gwarama, Kabare, Nyabibuye, n.k, kuna wananchi wamegeuka masikini tangu
hali hii ilipojitokeza miaka ya 1999 ambapo waliibiwa mifugo yao na
mali zingine tena kwa risasi za mirindimo!! Watu hawa hawakupata fidia
yoyote pamoja na juhudi kubwa alizozifanya Mkuu wetu wa Wilaya enzi
hizo, Col. John Mzurikwao!
Majambazi hawa wanatamba sana kwa sababu ya umbali wa kijiografia
ambapo matukio mengi hayatangazwi na wala hakuna waandishi wa habari
waliopo karibu!
Sasa hofu imekuwa kubwa kwani kuna uwezekano mkubwa wa majambazi
hawa toka Burundi kupata ushirika na wenzao wa upande wa Tanzania na
kuendeleza unyama huu!!
Naomba ndugu zangu kwa wale wenye mapenzi mema, watusaidie
kufuatilia jambo hili ili usalama uweze kurudi na wananchi waweze
kuendelea kufanya kazi zao kama kawaida.
Pamoja na juhudi kubwa za OCD wetu wa Kakonko, tunaomba detach za
JWTZ zirudishwe katika vijiji vya awali mpaka hapo usalama
utakapothibitika kurudi kama kawaida.
Naamini kupitia jukwaa hili pamoja na vyombo vingine vya habari, tutapata msaada stahiki.
Godfred B. Mbanyi
0786 571349
Chanzo:wanabidii
Post a Comment