MTANGAZAJI

TGNP YATAKA MAWAZIRI WANAOTUHUMIWA KWA UFISADI TANZANIA WAWAJIBISHWE


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
SERIKALI IWAWAJIBISHE MAWAZIRI WANAOTUHUMIWA KWA UFISADI
 
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unapenda kuwapongeza wajumbe   wa  Kamati za  Kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),  Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu, Ardhi Maliasili na Utalii kwa  kusimamia vema na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali zinazotokana na walipa kodi na kuwasilisha ripoti  zao Bungeni ambazo zimeibua uozo mkubwa na kujenga mjadala mpana unaotaka uwajibikaji kwa wanaohusika.
Tunawapongeza pia baadhi ya wabunge  walioshiriki katika mijadala  kwa kuzijadili ripoti hizo kwa undani bila kujali urafiki, itikadi za kisiasa,  hasa ile ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa  kuibua  uozo uliojificha na kusimamia maslahi ya Taifa.
Tumeshuhudia mara kadhaa kupitia vyombo vya habari  wabunge wakiacha itikadi zao za kisiasa na kusimamia kwa dhati dhana ya kushinikiza uwajibikaji katika vyombo vinavyohusika kutokana na ufisadi kama Richmond, Dowans nk. Hata hivyo, TGNP kwa muda mrefu  tumekuwa tukipinga ubadhirifu wa fedha za umma  na kudai haki ili kutokomeza ufisadi uliokithiri, lakini bado ufisadi umezidi kushamiri hasa katika Wizara  na taasisi za umma. Sisi kama wanaharakati tunasema kuendelea kwa ufisadi  ni aibu kwa serikali iliyoko madarakani, TGNP tuko mstari wa mbele  kushinikiza rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wote, hasa walioko pembezoni, kamwe hatutanyamazia aina yoyote ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya wananchi zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi
Tumeshuhudia wanawake na wasichana wakiendelea kuwa maskini na kukumbana na mifumo kandamizi kwa  kukosa haki za kufikia huduma za msingi kama vile   maji, barabara, afya, elimu, kilimo, utawala bora n.k. Fedha zinazopotea zinatokana na kodi za wananchi na jamii ina haki ya kuhoji uwajibikaji na wahusika wanatakiwa kuchukuliwa  hatua za kisheria.
 Tunawapongeza wabunge wote walioshiriki kwa dhati katika zoezi la kusaini kusudio la kutaka viongozi waliotajwa/kutuhumiwa  kwenye ripoti hizo kuwajibika.
Ili kuonesha dhana ya uwajibikaji na utawala bora unaozingatia misingi ya haki za binadamu, tunaitaka serikali kufanya  yafuatayo:
  • Kuwawajibisha mara moja Mawaziri, Manaibu waziri na watendaji wakuu wa serikali na mashirika ya umma ambao wametajwa kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma au kushindwa kusimamia rasilimali za Taifa.
  • Rais awafute kazi watendaji wanaotumia vibaya fedha za umma na kuwaongezea wananchi umasikini, ili iwe fundisho kwa watendaji wa serikali wenye tabia kama hiyo na wachukuliwe hatua za kisheria.
  • Serikali iboreshe mifumo ya kusimamia rasilimali za nchi yetu ili wananchi wote waweze kufaidi keki ya taifa kwa sababu mara zote serikali imekuwa ikisema Tanzania hatuna rasilimali lakini  hali halisi ni kwamba rasilimali za taifa zinaliwa na mafisadi wachache wa ndani na nje ya nchi.
 
Imetolewa na :
Anna Kikwa
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.