MTANGAZAJI

JAMII YATAKIWA KUACHANA NA VIUATILIFU

Jamii nchini imeaswa kuachana na matumizi ya viuatilifu (Pesticides) yasiyo ya lazima ya kuua visumbufu mashambani na majumbani mwao, ambayo yanasababisha madhara ya kwa binadamu ikiwemo ugumba, kuharibu mimba na vifo.
 
Badala yake jamii imehimiziwa kutumia njia mbadala zisizo na madhara kwa afya na rafiki wa mazingira.
 
Wito huo umetolewa jana na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili Dkt. Vera Ngowi kwenye mafunzo ya siku tatu ya kujenga uelewa wa athari za viuatilifu nchini na mbinu za ushawishi wa kutokomeza mlundikano wa viuatilifu hivyo na athari zake.
 
Mafunzo hayo yaliyohitimishwa karibuni mjini Kibaha mkoani Pwani yaliwashirikisha wawakilishi wa asasi zisizo za kiserikali zinazounda Mtandao wa Kupambana na Mlundikano wa Viuatilifu Chakavu hapa nchini (Africa Stockpiles Programme-ASP in Tanzania).
 
Dkt. Ngowi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao huo, alisema madhara yanayotokana na matumizi ya viuatilifu yamebainika kuwa ni makubwa na yanayozidi kuongezeka badala ya kupungua.
 
Alisema sababu kubwa zinazochangia kuwepo kwa athari hizo ni ukali wa sumu iliyoko kwenye viuatilifu hivyo na jamii kutofahamu matumizi sahihi na njia salama za uhifadhi wa viuatilifu ambako wengi wao wanahifadhi chumbani wanamolala na hivyo kuathirika kiurahisi.
 
Daktari huo ameyataja baadhi ya madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na sumu ya viuatilifu vinapoingia mwilini kuwa ni pamoja na ugumba kwa wanaume, kuharibu mimba ama kuzaa watoto wenye ulemavu, magonjwa ya ngozi, ini, mapafu, macho na hatimaye kifo.
 
“Watu wengi hawajagundua kuwa wanaathiriwa na viuatilifu hivyo kwa sababu madhara yake hayatokei papo hapo na wanapokuja kuugua wanadhani ni magonjwa ya kawaida na ndiyo maana pengine tatizo hili linaonekana kama siyo kubwa, ingawa kiuhalisia watanzania wengi wanapoteza maisha kwa tatizo hili,” alifafanua Dkt. Ngowi.
 
Alitolea mfano wa mazao ya mbogamboga yanayouzwa kwenye masoko mengi nchini zikiwemo nyanya, kabechi, mchicha, karoti, matango na nyingine nyingi zimewekwa viuatilifu vya kuua visumbufu shambani ambavyo wazalishaji hawazingatii kanuni za kiafya yaani muda wa kuzipeleka kwa mlaji baada ya kuwekwa viuatilifu.
 
“Kwa maana hiyo ukitafakari kwa makini utaona kuwa watu wengi wanaokula mboga zinazouzwa kwenye masoko yetu haya yakiwemo ya Kariakoo na kwingineko wanakula sumu zilizoko kwenye viuatilifu hivyo na ndiyo maana bidhaa kama hizi zinakataliwa kwenye masoko ya kimataifa kwa sababu wenzetu wanavifaa na wanapopima wanagundua usumu huo kwenye chakula,” alisema.
 
Kuhusu matumizi yasiyo sahihi daktari huyo alitolea mfano wa namna watu wanavyopuliza sumu ya kuua mbu majumbani pasipo kujikinga pamoja na watu wanaobeba mgongoni tenki la kunyunyiza sumu ya visumbufu mashambani na kwamba sumu hiyo mara nyingi huwavujia mgongoni na kuingia mwilini kwa kupitia sehemu za siri ambako ngozi yake ni laini na kusababisha ugumba hasa kwa wanaume.
 
Wakichangia kwenye mjadala huo, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliitaka serikali kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kutunga sera na sheria za kudhibiti athari hizo ikiwa ni pamoja na kuzuia kabisa uingizaji wa viuatilifu chakavu nchini.
 
Mwakilishi wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Bw. Susuma Susuma, alisema jamii na serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za shirika hilo za kuhimiza kilimo endelevu kinachotumia pembejeo za asili za kuua visumbufu mashambani na kuhifadhia mazao ghalani.
 
“Hii ndiyo njia pekee itakayowezesha nchi yetu kuepukana na athari za viuatilifu na kuokoa maisha ya watanzania wengi ambayo sasa yako hatarini, ninaishauri serikali na ninyi wenzangu tuunge mkono jitihada hizi za MVIWATA kwani sasa tunao wakulima wengi wa mfano wanaotumia kilimo endelevu na wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Bw. Susuma.
 
Kwa upande wake Bibi Huruma Muhapa, mkulima wa mfano anayetumia kilimo endelevu, kutoka kijiji cha Ibumila tarafa ya Makambako wilayani Njombe, alisema kutokana na utafiti alioufanya vitendo shambani kwake amethibitisha kuwa matumizi ya viuatilifu hasa sumu ya kuua magugu shambani, licha ya kuwaathiri kiafya pia yanawaongezea umasikini wakulima kwani huua vimelea vinavyorutubisha udongo na kwamba baada ya msimu mmoja wa kilimo shamba husika halitumiki tena kwa kukosa rutuba.
 
Madhara mengine ya viuatilifu yaliyobainishwa na washiriki wa mafunzo hayo yanatokana na uhifadhi mbovu wa viuatilifu ama vifaa vya kubebea viuatilifu huku wakitolea mfano wa wanafunzi 159 walionusurika kufa wilayani Serengeti, kifo cha mwanafunzi wilayani Muheza ambaye alikunywa pasipokujua kiuatilifu kilichowekwa kwenye chupa ya dawa ya kikohozi na kifo cha mtoto huko Sumbawanga ambaye alikula mandazi aliyokuwa ameyaweka kwenye mfuko wa nailoni (Rambo) uliokuwa umetumika kubebea kiuatilifu.
 
Washiriki hao pia waliitaka serikali kudhibiti mtindo unaozidi kushamiri wa kutumia vyombo vilivyoisha viuatilifu, kwa kuhifadhia vyakula na vinywaji aina mbalimbali kama vile maji, juice, asali kwani vinaongeza ukubwa wa tatizo.
 
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu katika wizara ya Kilimo na Chakula Bw. Gasana Rwabufigiri, alikiri kuwa viuatilifu vingi vinavyotumika kuua visumbufu ni hatari kwa afya ya binadamu kwani vinasumu kali.
 
Alisema kuwa katika baadhi ya maeneo wamelazimika kuacha kunyunyiza viuatilifu vya kuangamiza nzige kutokana na sumu hiyo kuingia kwenye maji ya mito yanayokwenda kwenye ziwa.
 
Mafunzo hayo yalienda sambamba na mkutano mkuu wa mtandao huo wa ASP ambao pamoja na mambo mengine ulipitisha Mpango Mkakati wa miaka mitatu (2012-2015) na kuidhinisha kamati tendaji iliyopo madarakani iendelee kwa miaka mingine mitatu ijayo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.