MTANGAZAJI

MAAFA YA MVUA DAR ES SALAAM - RAIS ATOA POLE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Mheshimiwa Said Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu 13 ambao
wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo
zimekuwa zinanyesha tokea jana, Jumanne, Desemba 20, 2011.

Aidha, Rais Kikwete amempa pole Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na

uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine za wananchi
uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa
miundombinu.Rais Kikwete pia ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es
Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo vyenye uzoefu wa maafa
kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya watu, kusaidia
waliozingirwa na mafuriko na kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote
waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Sadiq:

“Nimepokea kwa masikitiko habari za vifo vya wenzetu 13 vilivyotokana
na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo sote tumeishuhudia
katika Mkoa wa Dar es Salaam tokea jana. Nakutumia wewe rambirambi
zangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako kwa familia, ndugu na
jamaa waliopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko.
Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu, naelewa machungu yao na niko
nao katika hali ya sasa ya maombolezo.

Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia kwako kutoa pole zangu
nyingi kwa wote walioumia ama kupoteza mali zao katika mafuriko haya.
Wajulishe kuwa moyo wangu uko nao wakati huu wa mazingira
magumu.”“Chini ya usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa
kushirikiana na taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana
na majanga na dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea
kuokoa watu ambao bado wamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu
wale walioumia katika mafuriko hayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma
za kibinadamu wote waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafurikio
hayo.”

Imetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu,DAR ES SALAAM

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.