MTANGAZAJI

MAJADILIANO YA WAZI JUU YA ELIMU NA KUFUTA UJINGA

Mazungumzo ya kisera miaka 50 ya Uhuru: 
Hatua na mstakabali wa elimu na kufuta ujinga nchini Tanzania.

Taasisi ya Usomaji na Maendeleo ya E&D —Soma na Chama cha Wauza Vitabu wa Tanzania (BSAT) zinajihusisha na harakati za kufuta ujinga kwa njia ya kuhimiza usomaji na maendeleo ya vitabu. Dira ikiwa ni kuiona Tanzania ikitimiza malengo yake ya maendeleo kama ilivyojiwekea katika malengo ya milenia na MKUKUTA.Tunaamini jambo hili linaweza kufanikiwa kama tutatafakari kwa umakini mstakabali wa elimu yetu: falsafa, ruwaza, na utendaji kwa kuzingatia ubora, ushiriki, rasilimali, uendeshaji na vipaumbele inavyowekewa.

Katika kutimiza hilo, taasisi hizi zimeandaa, kama muendelezo wa Tamasha la VIitabu, mjadala wa wazi utakaofunguliwa jumatatu ya tarehe 28 Novemba 2011 na kufungwa jumatano tarehe 30 Novemba 2011 muda ukiwa ni saa 11:00 jioni hadi saa 4:00 usiku kwa siku zote ili kutafakari hatua zilizopigwa na wadau mbalimbali katika elimu na kufuta ujinga ndani ya miaka hamsini baada ya uhuru wa Tanganyika. Majadiliano haya yatafanyika katika viunga vya Mkahawa wa Vitabu Soma (Mtaa wa Regent Estate, Kitalu Na. 53, Mlingotini Close) kama sehemu ya Tamasha la Vitabu. Madhumuni ya majadiliano haya ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa elimu: wanajamii, waelimishaji, watekelezaji na watunga sera, wanataaluma, wanazuoni, pamoja na wanafunzi, kutafakari kwa kina kuhusu juhudi za wananchi na Serikali tangu enzi za Mwalimu Nyerere katika kufuta ujinga kama mojawapo ya maadui watatu wa maendeleo yetu.
 
Mdahalo utafanyika jumanne tarehe 29 Novemba 2011 huku ukihusisha tafakuri ya kina itakayofungamana na vionjo vya kisanaa, ukiwaleta pamoja wadau wenye stadi, mitazamo, na uzoefu mbalimbali katika elimu kuzungumzia hatua tuliyopiga katika maendeleo ya elimu na juhudi za kufuta ujinga. Maswali makuu yatakuwa: “kipi tumefanya vyema?”, “kipi tungeweza kufanya vyema zaidi?” na “nini tunahitaji kufanya?” ili ndani ya muongo mmoja tuweze kuwa mfano bora wa jamii inayojua kujifunza.

Mbali na hivyo, kuanzia jumatatu yatakuwa yakifanyika matukio kwa ajili ya jamii nzima kama vile maonesho ya vitabu na huduma za kielimu, vionjo vya kifasihi kama vile mashairi, ngonjera, ngano; shughuli za kuchangisha fedha kwa ajili ya huduma za kielimu ikiwemo ujenzi wa maktaba za jamii na mashindano ya fasihi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari, mnada wa vitabu vilivyotumika, maonesho ya muziki, dansi, nyama choma, na vinywaji.

Hivyo basi, tunatoa rai kwa jamii nzima na watu wote wahudhurie kwa wingi bila kukosa kwa siku zote tatu ili kuja kubadilishana mawazo na watu wengine wenye maono na mitazamo tofauti kuelekea kuboresha hali ya elimu nchini. Hapatakuwa na kiingilio chochote kwa siku zote tatu.

Demere Kitunga-(SOMA)                      Hobokela Magale-(BSAT)

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.