MTANGAZAJI

WARAKA WA GODBLESS LEMA MBUNGE WA ARUSHA MJINI KWA UMMA

Wapendwa wapiga kura wangu na Watanzania wenzangu.
Sina wakati mgumu kuchukua maamuzi haya yanayotokea leo. Upendo huu
nilio nao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya
maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi, rafiki zangu wametishwa, jamii
ya watu duni imeendelea kuishi kwa mashaka na matisho kwa muda mrefu.

Katika mazingira haya, nikawaza sana kuwa anatakiwa kutokea mtu mmoja

jasiri atakayeweza kuona thamani ya watu wengine. Huyo mtu anaweza
kuwa wewe lakini kwa wakati huu siwezi kumsubiri tena na nimechagua
kuwa mimi nikiamini kuwa utanikuta nikiendelea na safari ya ukombozi.

Tupo wengi sana tunaotaka mabadiliko, haki na ukweli. Hata hivyo hofu,

woga na mashaka yamepoteza thamani yetu yote ya maana ya kuishi.

Waliofungwa kwa kuonewa na kuteswa, waliokosa chakula na kulala nje,

waliokwenda hospitali na kukosa madawa, waliokosa ajira na kipato
mpaka kujikuta wametoroka familia zao, waliopoteza matumaini ya
maisha, waliopora utajiri wa nchi yetu kwa manufaa yao binafsi,
walionunua haki na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na kuwapora
vipato vyao vidogo na mashamba yao, USIULIZE SABABU NINI!

Nimetafakari sana na nikatambua kuwa sababu ni mimi pale nilipokuwa

kimya wakati wajane na wanyonge wanaonewa.

NIliposikia wengine wanaandamana kupinga uovu, uonevu, wizi, ufisadi

na ukandamizaji wa haki nikasema ni hao na wala sio mimi, kumbe
nilipaswa kuwa mbele katika harakati hizi.

Nilipoona wenzangu hawawezi kupata matibabu nikasema mimi sio mgonjwa,

nilipopata taarifa za rafiki zangu kufungwa kwa makosa yasiyo yao,
nilipoona watoto wa mitaani wanaomba chakula, nilipoona wazee
wamepoteza matumaini ya kuishi katika uzee wao, nilipoona vijana
hawana ajira, nilipoona mabinti wasichana wadogo wameamua kufanya
biashara ya ukahaba, NIKATAFAKARI,TENA NIKATAFAKARI, dhahabu zetu,
almasi yetu, Milima na mabonde yetu, Tanzaninte yetu, samaki wetu,
Uranium yetu, makaa ya mawe yetu, utalii wetu, ardhi na kilimo chetu
na zaidi utu na mahusiano yetu.

Na sasa siwezi kukaa kimya tena. NI afadhali vita inayotafuta haki na

usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Na
katika msingi huu hofu na mashaka vimekosa thamani kwangu, sitamwogopa
mtu yoyote, mwenye silaha yoyote, mwenye cheo chochote na wala
sitaogopa jela yoyote katika kupigania haki, utu wa kweli katika jamii
yangu.

Wanafikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha,

wanafikiri tutaendelea kuabudu uoga, wanafikiri wataendela
kutunyanyasabila sababu ya msingi LAKINI SISI TUNAJUA TUTASHINDA KWA
SABABU HAKI TUNAYOIPIGANIA NI MAKUSUDI YA MWENYEZI MUNGU.

Leo nitakwenda jela kwa hiari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa

NIA YA KUJITAFUTIA UTUKUFU WANGU bali ,” JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA
SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA
UTU WA BINADAMU.

Kila mara nilipotishiwa nikagundua wanaonitishia, wananitishia kwa

jela na mauti. Na mimi nikagundua na nikatambua ni afadhali kuishi
miaka hamsini jela huku sababu ikiwa ni kupinga uonevu na ukandamizaji
kuliko maisha ya woga na anasa yasiyo na kusudi katika kutetea utu na
heshima ya mwanadamu mwenzangu.

Wale mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na

wale mliobaki msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta
usawa katika nchi yenu.

Watakaotubeza na kututukana wasameheni kwani wanahitaji ukombozi wa

fikra, watakaotupongeza na kutuonea huruma wafundisheni ujasiri na
waambieni mapambano bado yanaendelea tunahitaji umoja wao. Nitarudi
mapema. MSIOGOPE, MSIOGOPE, MSIOGOPE , MUNGU YUPO UPANDE WETU.

Mhe Godbless Lema (MB) – Arusha Mjini 31 Oktoba 2011.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.