MTANGAZAJI

NILIVYOMLILIA KAWAWA

Mzee Kawawa hakuendekeza 'vijisenti'

NIWATAKIE heri ya mwaka huu mpya wa 2010 ingawa katika Taifa letu hili tumeumaliza mwaka uliopita na kuuanza huu kwa huzuni kuu-tumempoteza Mzee wetu, shujaa wetu na mshauri wetu, marehemu Rashid Mfaume Kawawa maarufu Simba wa Vita.

Kwa sababu hiyo, naamini msomaji wangu tutakubaliana kuwa yale masuala tuliyoyapanga kuyajadili awali, huu si wakati wake muafaka, ni vyema nami kama wachangiaji wengine nikamkumbuka Mzee Kawawa.

Nimesoma mengi yaliyoandikwa na wengi na si wakati wake mahali hapa kumueleza Mzee Kawawa alikuwa nani, alisimamia nini katika nchi hii, bali makala haya yataegama zaidi kuyaangalia maisha yetu baada ya kuondoka kwa Mzee Kawawa
.
Nilikuwepo Ikulu ya Dar es Salaam wakati Rais Jakaya Kikwete mmoja wa vijana waliokuzwa kimaadili na watu kama Mzee Kawawa, alipokuwa akilitangazia Taifa kifo cha Mzee wetu.Najua ilihitaji ujasiri kwa mtu wa aina ya JK kutangaza msiba wa mtu kama Kawawa.


Punde baada ya hapo, kigogo mwingine wa siasa za nchi hii, Kingunge Ngombare Mwiru, akazungumza pale pale Ikulu kuhusu Kawawa aliyemfahamu. Moja ya masuala yaliyonigusa ni pale Kingunge na hata Kikwete walipokiri kuwa watu kama Kawawa na hata Nyerere waliishi maisha ya mfano kisiasa na kijamii na ni juu ya sisi sote, hatuwezi kuwa kama wao, bali tunaweza kufanya yale mema na ya maana kwa Taifa kama yale waliyopata kuyafanya wao.

Siku na nyakati za maisha ya Mzee Kawawa zilijaa misukosuko na zaidi tamu na chungu nyingi. Alikulia katika kipindi kigumu cha ukoloni, Taifa likiwa chini ya wanyonyaji na kwa moyo thabiti hakukubali kubaki mnyonge.

Alikuwa mmoja wa viongozi hata kabla ya harakati za Mwalimu Nyerere, aliyediriki kuwaongoza wafanyakazi kugoma ili kushinikiza haki zao.

Kwa namna hii, aliishi katika nyakati hizo hata baada ya uhuru akawa mtu wa kuhakikisha ile chuki aliyokuwa nayo kwa wakoloni anaitafsiri kivitendo kwa kuhakikisha anahaha kuwa kiongozi wa kuwaletea watu wake maendeleo yaliyokuwa yamezuiwa zama za wakoloni.

Ndio maana katika kipindi chote alichokuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa, Mzee Kawawa aliishi maisha ya kawaida sana-hakulewa madaraka wala madaraka hayakumlevya.
Kawawa hakutumia madaraka yake vibaya kuwaibia watanzania kama tunavyoshuhudia hivi sasa. Kwa hilo moja tu kando ya mengine mengi, tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake.

Tumesikia ya vijisenti na kadhia nzima ya ubadhilifu wa mali za umma katika siasa za sasa jinsi wanasiasa licha ya kuwa na mamilioni na majumba ndani na nje ya nchi, wanavyotumia fedha hizo hizo walizokwiba kwa watanzania kuwanunua ili wapewe madaraka makubwa ili wakale tena.


Baadhi ya Watanzania wamekuwa wakitoa maoni na kumtaja hayati Edward Moringe Sokoine kuwa ndiye Waziri Mkuu bora kabisa ambaye mpaka sasa haijapata kutokea mtu kama yeye katika siasa za nyakati zake kwa ufuatiliaji.

Mimi sipingani na hilo, lakini nasema kwa utulivu wa kutokuwa na papara katika kuyaendea mambo na kutokuwa na tamaa,fitina wala kiroho papo, Mzee Kawawa alikuwa jabari tutakaloendelea kulitumia kama ngao ya kuwapima na hata kuwakataa waendekeza vijisenti.

Safu hii inakumbuka jinsi enzi za Mwalimu Serikali ilivyokuwa ikitoa maamuzi magumu sana na Kawawa ndiye aliyekuwa akitekeleza kwa kuyasimamia huku akikubali lawama zote kwa yale yaliyokuja kugeuka kuwa mamuzi mabovu.Hakuwahi kumtaja kiongozi mwingine na kumlaumu kwa sababu ya yeye kulaumiwa.Bali alikuwa mvumilivu na aliyakubali yote.

Wengi wanakumbuka kuwa Mzee Kawawa alishikiri katika kusimamia maamuzi magumu sana ili kuiokoa nchi, alikuwa mtu wa watu na alikuwa mtetezi wa kila mtu bila kujari matabaka na tofauti na wanasiasa wengi hasa wasaidizi wengi wa Marais wa sasa, hakuwa akitenda yote hayo ili siku moja awe Rais-alilenga kuwatumikia watu na kuona wakiendelea basi.

Inasikitisha leo, baadhi ya viongozi wanapewa nafasi ya kuwa washauri wa Rais wetu lakini ndani yake wanafanya yao ya kujinufaisha na kujijenga. Kawawa angetaka hayo angekuwa Rais baada ya Nyerere. Hakuwa wa kujikweza.


Baadaye Serikali yake na ya Nyerere ilipompata mtu mkali zaidi wa kuwasaidia, hayati Edward Moringe Sokoine, wahujumu uchumi wakati huo walibanwa sana na hakuna aliyethubutu kuiibia nchi yetu na aliyefaulu kuiba alipokonywa mali na kushitakiwa tofauti na sasa wezi wa fedha za umma wanabembelezwa na kupewa muda warudishe fedha.

Yeye na Mwalimu Julius Nyerere mbali na kutotaka masihara kazini walionyesha maisha ya kutojilimbikizia mali. Mzee Kawawa alipotoka madarakani wanaomfahamu wanasema hakuwa na kitu na kama si sheria za pensheni kwa wastaafu, angeweza kuwa mmoja wa watanzania wa kusaidiwa kwa michango ya ndugu ili apate kutibu afya yake iliyokuwa ikidorora licha ya kupatakuwa kiongozi mkuu kitaifa.

Ndio maana aliweza kwenda kuishi eneo kama Madale, nje ya Dar es Salaam na si Oysterbay au Masaki-Kawawa hakuwa na uwezo wa kujenga sehemu hizo ambako mawaziri wakuu wa miongo hii wamejenga, tena kabla hawajafika alipofika, walishakuwa wamejenga mahekalu.

Ndio maana kwa kutambua mchango wake kwa Taifa ama kwa kupigania utawala bora na haki za watu moja kwa moja au kwa yeye kujinyima na kuwa mfano bora, Januari mwaka 2007, Kawawa alitunukiwa tuzo ya Dk. Martin Luther King.

Viongozi wetu wengi wa sasa wanakosa sifa muhimu ya kiuadilifu kwa wananchi wao na si ajabu tuzo kama walizopata akina Mzee Kawawa zikaendelea kuwa adimu nchini katika miaka ijayo labda zile za watu kuzifadhili na kisha kujitunukia wenyewe.

Moja ya maneno yanayoweza kubaki kuwa wosia kwetu ni yale aliyoyasema wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo ambapo kwa kuwa nilikuwepo wakati akikabidhiwa pale kwenye ubalozi wa Marekani niliiona ari aliyokuwa nayo kutamani kuendelea kutoa mchango wake kwa Taifa ingawa nguvu hakuwa nazo tena kutokana na umri.


“Heshima iliyotukuka mliyonipa si tu imeniletea faraja, bali pia ni kichocheo cha kuendelea kuwatumikia Watanzania pale ambapo nitaweza kuwatumikia bila kujali itikadi zao za kidini au za kisiasa, kwa manufaa ya taifa kwa ujumla,” alisema Kawawa na kuongeza:
“Sasa nafuga nyuki na nipo tayari kumfundisha mwenzangu yeyote ufugaji wa nyuki wa kisasa,” alisema akieleza maisha yake baada ya siasa kuwa ni ya ukulima.


Pia katika hotuba yake hiyo aliasa viongozi na wanasiasa akisema: “Naomba mtupie macho makundi madogo madogo ambayo sauti zake hazijasikika, yapatiwe misaada ili yapate uwezo wa kujikwamua kiuchumi, yapate fursa sawa katika jamii ili uwezo walionao utumike kuleta maendeleo.” Hiki alichokisema hapa sijui kama kimetimizwa hadi mauti yalipomfika Ijumaa iliyopita saa tatu na dakika ishirini asubuhi.

Ni wazi kuwa Mzee Kawawa katika siku zake za mwisho za maisha alikuwa na dukuduku jingi moyoni hasa kutokana na mwenenzo wa siasa za nchi na hasa ufisadi na kamwe hakufa akisononeka moyoni, alipata kusema hadharani na waliochukia walichukia.
Alitoa dukuduku lake wakati akizindua kitabu kiitwacho 'CCM na Mustakabali wa Nchi Yetu’, kilichoandikwa na Makwaia wa Kuhenga aliposema:

“Hatupendi kusikia jambo la ulimbikizaji wa mali, wanaofahamika watajwe hadharani na waeleze fedha hizo wamezipatapataje na wamezipata wapi,” alisema Kawawa.


Alisema kuwapo kwa mafisadi ndani ya chama tawala ni jambo la hatari ambalo linaweza kukiweka chama hicho katika wakati mgumu.

Amewataka wana CCM kutambua kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hakuwa mtu mwenye tamaa ya kujilimbikizia mali, hivyo changamoto hiyo haina budi kuzingatiwa.
“Mimi sikuwa na mabilioni ya fedha, hivi ningeyapata wapi? Mwalimu Nyerere hakuwa mtu mwenye tamaa, hata hakujilimbikizia mali, hii iwe ni changamoto kwa wana CCM.”


Akaendelea kufafanua kuhusu tabia ya kukosoana katika mambo ya chama na Serikali ambayo kwa baadhi ya watawala wa sasa imeanza kuonekana kama ni uhaini kufanya hivyo alisema:
“Yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki ni changamoto kwa viongozi wa chama chetu, tunapojadili mambo mazito kama yaliyomo katika kitabu hiki, tunatakiwa kuwa watulivu na wenye kutanguliza mbele uzalendo na utaifa wetu.”


“Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981 ulitamka bayana kwamba kujikosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi, alichofanya Makwaia wa Kuhenga ni kukikosoa chama na Serikali yake, hii ni changamoto ya kushiriki mjadala utakaoelekezwa kuimarisha ujenzi wa taifa letu.”

Na zaidi Mzee Kawawa ameondoka akiwa ameliachia Taifa urithi mmoja muhimu-alikubali katika siku za mwisho za maisha yake, kukubali kuandikwa maisha na harakati zake. Huu ni urithi mzuri, tukitafute na kukisomea kitabu chake kilichoandikwa na Dk. John Magoti, kiendelee kuturiwadha kuhusu siku na maisha ya Simba wa Vita.

Mwandishi ni Mhariri wa gazeti la KULIKONI na anapatikana kupitia simu
:0713 584467 au
baruapepe:hassanartist@yahoo.com.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.