MTANGAZAJI

KUFUTIWA USAJILI WATAHINIWA WA KUJITEGEMEA

Mitihani ya darasa la saba tayari imefanyika na wengi wa wazazi sasa wanahaha kuona kwamba watoto wao wanaingia shule nzuri za sekondari ili waendelee na masomo yao na hatimaye kuingia katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Kama ilivyo kawaida, mitihani hii haiamshi sana hisia za watu kwa vile hata vyeti hivi, ambavyo vimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili, havithaminiwi na mwajiri wala shule yoyote ya sekondari wala chuo. Ni kama lugha yenyewe ya Kiswahili na mswahili mwenye wasivyothaminiwa. Matukio ya wizi wa mitihani yapo lakini si mengi kwa vile kufaulu au kushindwa katika mitihani hii hakuna athari yoyote kwa mtahiniwa.

Sasa macho na msikio ya watanzania wote yako kwenye hii mitihani ya kumaliza kidato cha nne ambapo mwanafunzi, kwa mara ya kwanza, atafanya mitihani yote kwa lugha ya kizungu na hatimaye kupewa cheti kilichoandikwa kizungu na kitakachothaminiwa na watu wote wakiwemo hata mende na panya waishio nyumbani. Ni cheti ambacho sasa kitaanza kuonyesha kwamba huyu ni “Mzungu mweusi” ambaye ndege ilijaa tu na hivyo akaahirisha safari yake ya kurudi kwao Ulaya.

Mitihani ya kidato cha nne itafanyika kuanzia Oktoba 05 hadi 23, 2009. Mitihani hii hufanyika kwa mbwembwe za aina yake, utadhani ni harakati za wabunge za kampeni ili wapate kura na kuingia katika ulaji kutokana na kusinzia Bungeni huku miswada mibovu ikipitishwa kama sheria na kuimaliza nchi yetu. Kila mbinu chafu hutumika ilikuhakikisha tu kwamba mwanafunzi anafaulu kuendelea na masomo.

Kama ilivyo kawaida, kila mtahiniwa hujitahidi kwa kila njia kuona kwamba anafaulu mitihani hii. Karibu kila mmoja hujisomea na kuhakikisha kwamba analenga kupata alama za juu ili cheti chake kifae kama sifa za kuingia kidato cha tano na hatimaye vyuo vya elimu ya juu. Kwa wenzangu mie ambao wanajijua kabisa kwamba aidha ni bongolala au wale ambao wamesomea shule zisizo na walimu wala vifaa vya kufundishia, hujitahidi kuwa karibu na wale wataosimamia mchakato mzima wa mitihani ili waweze kuiba hiyo mitihani.

Wengine ndio wale tunaowasema kila siku ambao wamesomea katika vituo visivyosajiliwa na wizara ya elimu ambavyo hujibadilisha majina na sehemu kila uchao; utadhani kinyonga. Jana kiliitwa “tuisheni”. Leo kinaitwa “Mbuyuni sekondari” na kesho utakuta kinaitwa “Baobab Sekondari”. Ili mradi tu kuwarubuni wateja kwamba hiyo shule ni “British” na si ya Kiswahili swahili iliyojaa ubabaishaji na mizengwe. Kama watanzania walivyo na kasumba ya kupenda vya wazungu, wengi wa vijana wetu, na hata watu wazima, hurubunika na kuanza kusomea katika vituo hivyo vinavyopika wasomi “Vihiyo”.

Juma lililopita, tumemsikia waziri mwenye dhamana ya elimu Mh. Prof. Jumanne Maghembe akitangaza kwamba, jumla ya watu 100,400 waliomba kufanya mtihani wa kidato cha nne kama watahiniwa wa kujitegemea. Katika hawa, jumla ya waombaji 3,034 (3%) walinyimwa usajili kutokana na kujaza taarifa za uongo (80%), kukosa namba za mitihani ya kidato cha pili (9%), kukosa kujaza masomo (1%), kuandika vituo hewa (11%).

Sababu zingine ambazo waziri alizitaja bila kutoa takwimu ni sifa za kughushi na watu kujaziwa fomu na ndugu zao.Tafsiri ya takwimu hizi ni kwamba waombaji wengi wamenyimwa usajili kutokana na udanganyifu unaotokana na wao wenyewe au wamiliki wa vituo walivyoandikisha. Hii inachukua asilimia 91 ya sababu zote za waombaji kuzuiwa kufanya mitihani ya kidato cha nne kama watahiniwa wa kujitegemea kwa mwaka huu. Japo waziri hakufafanua kwamba ni udanganyifu wa aina gani, ni wazi kwamba sehemu kubwa ya udanganyifu huu ni katika ujazaji wa Taarifa za maendeleo (continuous assessments – CA).

Sababu nyingine ni kwa hawa waombaji kujaza vituo ambavyo havikusajiliwa. Ni wazi kwamba watahiniwa wa namna hii ni wale waliosomea katika vituo visivyosajiliwa ambao, kwa kuona kwamba serikali yetu haichukui hatua yoyote, walidhani kwamba vituo hivyo vinatambuliwa na serikali. Ni kama tu ilivyokuwa kwa DECI ambapo wavujajasho walifyonzwa vijisenti vyao mpaka jamaa wa DECI wakashiba ndipo serikali ikazinduka na kuifungia.

Ni kama tu inavyokuwa hata katika mashule haya yanayoungua moto na kuteketeza wanafunzi utadhani ni mabua yanayochomwa shambani ili kuliandaa kwa msimu wa kilimo unaofuata.

Tumeona watu wametapeliwa pesa na muda wao lakini hatutegemei wizara kuchukua hatua yoyote kwa hawa matapeli wa vituo hewa zaidi ya kuwaliza hawa maskini waliotapeliwa. Kwa hakika wizara inawajua lakini haiwachukulii hatua yoyote pengine kwa sababu ya minong’ono inayoendelea kwamba kuna mikono ya wakubwa humo. Kama minong’ono hii ni ya kweli, basi pole kwa wote waliofanyiwa unyama huu. Kurunzi inaamini kwamba ipo siku serikali nyingine itakuja na kuwafuta machozi yao yote.

Ninaungana na waziri wetu katika kuona kwamba, ni wale tu wenye sifa za kufanya mtihani ndio wanaoruhusiwa kuingia katika vyumba vya mitihani na wote wasio waaminifu wanaondolewa na kuhakikisha kwamba hawafanyi mtihani tena kwa sababu, kwa kuwapa upenyo wa kufanya mtihani baadaye, tunatengeneza kizazi cha wezi, matapeli na mafisadi.

Pamoja na pongezi hizo, kurunzi inapenda kutoa maangalizo kadhaa na hatimaye kutoa ushauri wa kuhakikisha kwamba haya maswala ya udanganyifu hayatokei tena katika historia ya nchi yetu.

Kwanza ni kuhusu huu utaratibu wa mtahiniwa kupeleka taarifa zake za maendeleo mwenyewe kule NECTA. Hii ni teknolojia ya kizamani sana haitegemei wizara isimamiwe na Profesa halafu akubali teknolojia hii kongwe itumike wakati teknolojia rahisi, zenye ufanisi mkubwa zaidi na zenye gharama nafuu zipo.

Ninatambua fika kwamba Profesa Maghembe ni msomi mbobevu mwenye shahada ya uzamivu aliyoipata kwa kusoma, kufanya utafiti wa kisayansi na kutoa mihadhara katika vyuo vikuu kadhaa ndani na nje ya nchi yetu. Huyu si mbabaishaji hata kidogo.

Hivyo hatukumtegemea kabisa kutamka kwamba amefutia usajili mwombaji kwa vile amejaza taarifa za uongo. Mwanya huu wa kujaza taarifa za uongo umetokana na wizara yenyewe kuruhusu matumizi ya teknolojia ya kizamani wakati teknolojia za kisasa zipo na zinatumika katika Baraza la mitihani (NECTA).


Kutokana na angalizo hili, ninapendekeza kwamba, kila mwanafunzi anayesajiliwa shuleni awe na namba ya kudumu ya usajili kama ilivyo kwa kila mlipa kodi ambaye mamlaka ya kodi (TRA) humpatia namba ya utambulisho wa mlipa kodi (taxpayer identification number – TIN). Namba hii itumike kujaza takwimu zake za maendeleo kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu. Namba hii iwekwe katika mkekatakwimu (database) wa NECTA.

Katika mkekatakwimu huu, taarifa zote za maendeleo ya mwanafunzi ziwekwe. Kama utaratibu huu utafuatwa, hapatakuwa tena na haja ya mwanafunzi kujaziwa taarifa ya matokeo na mkuu wake wa kituo cha kufanyia mtihani kwani taarifa zote zitakuwa zipo NECTA. Atakachojaza kwenye fomu ya maombi ni namba yake ya usajili, picha yake na wasifu wake (curriculum vitae - CV). Hata mwanafunzi anayeomba kuingia chuo cha elimu ya juu au kuomba ajira, hatakuwa tena na haja ya kupeleka vyeti vyake zaidi ya CV yake.

Pendekezo la pili ni kwa NECTA kuwa na mapenzi na wadau wake. Kurunzi inaiomba NECTA kuwa na muda wa kuzungumza na wadau wake hata kabla ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari. Kujiweka mbali na wadau wake ni kutengeneza ukuta utakaozuia mawasiliano yatakayolenga katika kushauriana na kuondoa kasoro hizi tunazozipata kupitia vyombo vya habari.

Pendekezo la tatu ni kwa wizara ya elimu na serikali kwa ujumla kuachana na mtindo wake wa kukurupuka wakati mambo yanapoharibika. Badala yake itumie muda mwingi kuzuia mambo yasiyofaa yasitokee. Kuwanyima usajili waombaji waliotokea katika vituo visivyotambuliwa ni hatua ya lazima lakini isiyojitosheleza.

Haitoshi tu kuwanyima usajili watu waliosomea katika vituo hivi na, kwa kweli, ni uonevu wa aina yake kwa vile waliokuwa wakisomea hapo walijua kwamba vituo hivyo vinatambuliwa na serikali. Mojawapao ya mbinu za kudhibiti utapeli huu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vinavyotoa elimu vinasajiliwa na hivyo kuwa rahisi kuviratibu. Japo sijafanya utafiti wa huu udanganyifu huu, inaamini kabisa kwamba umetokana na watu wenye tamaa ya pesa wanaotapeli watu.

Kama vituo hivi vitadhibitiwa, basi ni wazi kwamba udanganyifu utatoweka kabisa.
Suala la usimamizi wa elimu ni nyeti kwa vile ndilo linalotoa dira ya maendeleo ya nchi yoyote duniani. Endapo elimu yetu itasimamiwa kwa ukamilifu, ni wazi kwamba nchi yetu itajikomboa kutoka makucha ya maradhi na umaskini yanayotufanya kuaibika katika ulimwengu huu wa utandawazi na kutufanya kuwa ombaomba hata wa chakula japo nchi yetu ina utajiri wa kila aina.


Mwandishi ni mmiliki wa shule na mshauri wa kujitegemea katika maswala ya usimamizi wa elimu. Pia ni katibu mkuu wa chama cha wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali (TAMONGSCO) na ni mjumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC). Anapatikana kwa namba 0715/54/84-316570 au baruapepe tamongsco@yahoo.com

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.