MTANGAZAJI

KILIMO NA UWEKEZAJI NCHINIMaonesho ya nane nane yamekuwa yakifanyaika kila mwaka hapa nchini je yanawanufaisha vipi wakulima na wafanyabiasha wa mazao kama haya ama yanawanufaisha viongozi na yanatumika kama propaganda??? sasa hivi kila kiongozi anapigia chapuo uwekezaji

DHANA YA UWEKEZAJI
Hakuna nchi yoyote duniani ambayo imeendelea bila uwekezaji. Kwa ufupi kabisa, uwekezaji unamaanisha jitihada za kugeuza mali asili za nchi kuwa katika rasilimali kwa kutumia nyenzo kama mtaji, teknolojia na nguvukazi.

Ziada inayotokana na uzalishaji hurejeshwa katika kuimarisha miundombinu, mitaji, teknolojia na rasilimali (watu, fedha, malighafi) ili faida iweze kupatikana na pale inapopatikana faida ndipo matunda ya mandeleo huonekana kwavile faida hiyo hutumika kukidhi mahitaji ya muhimu na ya ziada kwa mwenye mali au aliyewekeza

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa kawaida uwekezaji hufanywa na kundi dogo katika jamii zinaonyesha kuwa, zaidi ya 70% ya wakazi wa nchi kusini mwa jangwa la Sahara hujishughulisha na kilimo kwaajili ya kujikimu na siyo cha uwekezaji
Wakulima hawa wadogo ndio huchangia zaidi kwenye pato la taifa kuliko wakulima wakubwa na wawekezaji kwenye kilimo.

Tangu wakati wa ukoloni hadi baada ya uhuru miaka ya 60, 70 na 80, serikali nyingi za Kiafrika zilibeba jukumu la kiuchumi ambalo hata hivyo zililazimika kuliacha kwa sekta binafsi kuanzia katikati ya miaka ya 1980.

Uwekezaji katika ardhi ya Tanzania

Tanzania ina ukubwa wa zaidi ya km2 940,000 za , na bila shaka uwekezaji hufanyika katika ardhi kwa sehemu kubwa.

Kwa mujibu wa sheria za ardhi na.4 na 5 za 1999 ardhi ya Tanzania imegawanyika katika makundi 3 ambayo ni ardhi ya Jumla, ya kijiji na ya hifadhi.
Hadi sasa ardhi ya hifadhi inaelezewa kufikia zaidi ya 30% ya ardhi yote
Ardhi yenye rutuba na inayofaa kwa kilimo cha aina mbalimbali inakadiriwa kufikia hekta milioni 80 eneo linalotumika kwa sasa linakadiriwa kufikia asilimia 6 hadi 10 ya eneo hilo. Licha ya kuwa hakuna mpango bora wa matumizi ya ardhi wa kitaifa inamaanisha ardhi ipo ya kutosha kwaajili ya uwekezaji.

Ardhi na uwekezaji

Shughuli za uwekezaji huongozwa na sheria ya uwekezaji ya 1997. Hata hivyo, sheria ya ardhi inatamka wazi kuwa wasio raia wa Tanzania hawarushusiwi kumiliki ardhi isipokuwa kwa matumizi ya uwekezaji ambapo hupewa hati hafifu kupitia kituo cha uwekezaji (TIC).

Hata hivyo, imeshuhudiwa mara nyingi wawekezaji wasio watanzania wakimiliki ardhi, wakiwaondoa wamiliki wa asili katika maeneo yao na kuharibu kabisa mifumo yao ya maisha.

Hii mara nyingi imetokea kwasababu ya kukiuka makusudi sheria na taratibu zilizopo, udhaifu wa mifumo ya utekelezaji wa sheria na dharau kwa vyombo vya ngazi za chini za utawala na wananchi wao kwavile maamuzi hufanywa ngazi za juu.

Sekta zilizovutia wawekezaji

Ingawa karibu kila eneo limevutia wawekezaji wa aina fulani, katika ardhi maeneo matatu muhimu yameonekana kuvuta zaidi wawekezaji
Maeneo hayo ni Uchimbaji madini, shughuli za wanayamapori (uwindaji, mahoteli, utalii) na kilimo.

Katika kilimo ambako kuna wazalishaji wadogo, mlengo wa hivi karibuni umekuwa kwenye kilimo cha nishati uoto kwaajili ya mafuta ya magari na mitambo.

Licha ya kutolea mifano kutoka sekta nyingine, mada hii inaangalia zaidi hali halisi ya uwekezaji katika sekta hizi tatu na athari zake kwa mzalishaji wa kawaida.

Tathmini ya uwekezaji

Kumekuwa na ongezeko la wawekezaji tangu miaka ya 1980’s milango ilipofunguliwa, wengi wanatoka nje ya nchi mf. S/Afrika, Kenya, UK, (japo wengi si katika kilimo bali mawasiliano, fedha, utalii n.k)

Katika kilimo, uwekezaji umeanza kuongezeka si zaidi ya miaka 10 hadi 15 iliyopita baada ya mashamba yaliyokuwa yameachwa na serikali kuanza kufufuliwa kwa njia ya ubinafsishaji (NAFCO …Hanang, Mbarali, NARCO…Kitulo, Mkata)

Pia kupanda kwa bei za mafuta na chakula duniani kunatajwa kuongeza kasi ya uwekezaji katika kilimo

Wawekezaji wengi sasa wanaenda vijijini kutafuta ardhi wenyewe baada ya kupewa na Kituo cha Uwekezaji kama sheria inavyotaka

Kutokana na wanavijiji kutokuwa na uwezo wa kimaarifa na ujuzi wa kujadiliana na wawekezaji kwa mizania sawa, wamekuwa wakitoa ardhi bila kufuata taratibu za kisheria (mf. Mikutano mikuu ya vijiji kutoidhinisha au kuidhinisha kwa mashinikizo ya ngazi za juu)

Pale ambapo wanavijiji wamethubutu kuhoji, sheria imetumika vibaya kuwapora ardhi na haki yao. Mf. Ardhi ya kijiji isiyotumika wala kukaliwa inaelezewa na sheria ya ardhi namba 4 kuwa ni ardhi ya jumla na hivyo kuchukuliwa na serikali kuu wakati wowote ingawa kwa hali halisi ni ardhi ya kijiji.

Kwa ujumla, kumekuwa na mijadala mingi kuhusuana hasa na tija iliyotokana na uwekezaji kwavile kwa sehemu kubwa umeonekana kunufaisha watu wachache hususani wenye fursa ya kushindana kiuchumi na kuwaacha wanavijiji walio wengi nje ya mfumo.
Kumekuwa na maswali pia juu ya viwango na manufaa ya kodi inayolipwa na wawekezaji kuwa hailingani na thamani halisi ya rasilimali walizowekeza na hivyo haikidhi huduma za kijamii

Manufaa ya uwekezaji mkubwa katika ardhi wa wazalishaji wadogo.
Kukuza uchumi. Kumekuwa na madai kuwa uwekezaji umekuza uchumi mkuu kwa kiwango cha kati ya 5.2-7% lengo likiwa kufikia zaidi ya 10% lakini ukuaji huu umelalamikiwa kutoleta matokeo katika hali halisi ya maisha ya wananchi wa ngazi ya jamii.
Kitendawili hiki kinahitaji kuteguliwa la sivyo kuna tatizo katika mfumo wa jinsi pato la uchumi mkuu linavyohusishwa maisha halisi

Kuongeza fursa za ajira. Kwa sekta ya madini inasemekana kuwa kufikia mwishoni mwa miaka ya 90, watu kati ya 500,000 na 1.5mil walipata ajira. Hata hivyo, taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya ajira 1,000,000 zimepotea katika sekata ya madini tangu uwekezaji mkubwa uliporuhusiwa nchini.
Kufikia mwaka 2006, taarifa iliyotolewa na benki ya dunia inaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na wachimbaji wadogo 170,000 ikiwa ni pungufu ya karibu ya mara tatu ya waliohamishwa wakati mgodi wa Bulyanhulu unafunguliwa

Ongezeko la kipato kwa wazalishaji wadogo mf. Wakulima wa miwa Mtibwa hadi mwaka 2006 walikuwa wanachangia takribani 56% ya malighafi inayotakiwa kiwandani
Ongezejo la mauzo nje ya nchi na fedha za kigeni. Lakini ni nani ananufaika na hiyo biashara ya nje?

Ongezeko la pato la taifa kupitia kodi mbalimbali, pia mirahaba na gawiwo. Mf. Dhahabu 3% Almasi na vito 5%
Kukua kwa soko la mazao ya wazalishaji wadogo Mf. Miwa
Kuboreka kwa miundo mbinu na huduma za jamii kama barabara, mashule, mawasiliano n.k
Kuboreka kwa teknolojia katika uzalishaji.

Athari za uwekezaji katika ardhi kwa wazalishaji wadogo

Uharibifu wa vyanzo vya maisha (destruction of means of livehoods), ukulima, ufugaji, uwindaji, uchimbaji na uvuvi wa asili vimevurugwa na uwekezaji kwa namna mbalimbali. mf,. Zaidi ya ajira 500,000 zilipotea Bulyanhulu mwaka 1996 mgodi ulipofunguliwa. Hao walikuwa ni wachimbaji wadogo na watoa huduma kwa wachimbaji hao wakiwemo mama lishe .n.k

Uhaba wa chakula. Ardhi inayofaa kuzalisha chakula inatumika kuzalisha malighafi zisizoliwa na wazalishaji wa chakula kukimbilia kutafuta vibarua katika maeneo mapya ya uwekezaji (mf.Migodini, utalii kwenye maeneo ya wanyamapori n.k) hadi 2007 zaidi ya hekta 641,000 wamegawiwa wawekezaji wa nishati uoto. Ardhi hii ingetumika kuzalisha chakula.

Wananchi kuondolewa katika ardhi yao bila fidia au kwa fidia kidogo. Mf. Kaya 86 ziliondolewa kupisha mgodi wa Geita katika kijiji cha Mtakuja na watu zaidi ya 250 hawana pa kuishi kwa takribani miaka miwili sasa

Wananchi wa kijiji cha Namwawala Kilombero wako hatarini kuondolewa kijijini kupisha mwekezaji asiyejulikana. 62% ya ardhi yao 9272.54ha zinachukuliwa na kuathiri zaidi ya wakazi 10,000 na watoto wa shule 200

Uwekezaji katika hifadhi za wanyamapori umeondoa wananchi wengi katika maeneo yao ya asili mf. Vijiji kadhaa ndani ya Loliondo GCA, wamechomewa nyumba na mazao ili wampishe mwekezaji wa uwindaji OBC

Pia eneo la Sukenya wilayani Ngorongoro, na Vilima vitatu Babati unyanyasaji umetokea kwa viwango vya kutisha

Fidia kidogo isiyoendana na viwango vya soko. Mf. Kakola wilaya ya Kahama walilipwa kati ya sh.35,000 na 200,000 tu kupisha mgodi wa Bulyanhulu.

Taratibu za kulipa fidia kukiukwa na wadai wengine Mara Nyakabale, kati ya wadai 110waliolipwa ni 39 tu huku 71 wakiendelea kusubiria bila matumaini ya kulipwa

Ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mf. Zaidi ya wachimbaji 50 wanasadikiwa kufukiwa hai katika mgodi wa Bulyanhulu 1996,taarifa za mauaji ya mara kwa mara migodini mf. North Mara, Mererani, wachimbaji kupita katika mashine za mionzi wakiwa uchi hali inayohatarisha afya zao tumeisikia juzi bungeni n.k

Uharibifu wa mazingira mf. Mgodi wa North Mara maji yenye sumu kutiririkia mtoni, Athari za kimazingira kwa mradi wa magadi lake Natron, Hoteli ya Serengeti na mkondo wa wanyamapori n.k

Migogoro juu ya matumizi ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji. Karibu kila siku kuna taarifa kwenye vyombp vya habari juu ya hili. (Kilimo cha mibono kaburi kwenye ardhi ya chakula) mf. Mbarali, Rukwa, Rufiji, Kisarawe

Uharibifu wa ikolojia na baoanuai. Mf. Ufyekaji wa misitu ukanda wa tao la mashariki kwaajili ya mashamba makubwa km vile Kilwa, Bagamoyo, Wami na Pangani. Pia hoteli za ufukweni kama vile Mafia, Kigamboni na Bagamoyo na ustawi wa mikoko na mazalia ya samaki kwaajili ya wavuvi wadogo

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.