MTANGAZAJI

VIONGOZI WA WAADVENTISTA WAKUTANA NA RAIS WA SELYCHELLES


Viongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Seychelles wamekutana na Rais Patrick Herminie  katika Ikulu ya nchi hiyo Agosti 25, mwaka huu kujadili namna kanisa linavyoweza kusaidia kukabiliana na changamoto za kijamii zinazolikabili taifa hilo, hususan tatizo la dawa za kulevya.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Rais, Ujumbe huo uliongozwa na Mchungaji Ntep Ntep, Mwenyekiti wa Unioni Misheni ya Seychelles, akiwa na Katibu Mkuu Mchungaji Theophile Tefison, Mhazini Mkuu Hugh Watts, na Garry Woodcock, mwanafunzi wa thiolojia anayejitayarisha kwa huduma ya uchungaji.

Mazungumzo yalijikita zaidi kwenye nafasi ya familia imara katika kukabiliana na changamoto za kijamii zinazolikabili taifa la Seychelles, hususan tatizo la dawa za kulevya, na jinsi kanisa linavyoweza kuunga mkono jitihada za serikali kupitia kinga, msaada wa kifamilia na miradi ya kijamii.

Miongoni mwa mipango iliyojadiliwa ni kuanzishwa kwa kituo cha familia nchini Seychelles. Kituo hicho kinapendekezwa kutoa msaada kwa familia na kuimarisha msingi wa kifamilia kuwa nguzo ya jamii, huku kikisisitiza kinga na hatua za mapema kabla matatizo hayajawa makubwa.

Ujumbe huo pia ulieleza kazi ya kanisa hilo katika kusaidia familia na jamii, ikijumuisha miradi ya Praslin na La Digue, na kuonyesha utayari wa kushirikiana na serikali katika maeneo ambayo uzoefu wa kanisa unaweza kuleta mabadiliko.

Rais Herminie alikaribisha ushirikiano huo, akibainisha kuwa tatizo la dawa za kulevya bado ni changamoto kubwa inayohitaji sekta mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja. Alisisitiza umuhimu wa kupunguza mahitaji ya dawa za kulevya huku vijana wakipewa njia mbadala chanya, vielelezo vya kuigwa na matumaini ya maisha ya baadaye.

Mkutano huu unaendeleza uhusiano uliopo kati ya viongozi wa kanisa na serikali ya Seychelles. Mwaka 2022, ujumbe wa Idara ya Huduma za Wana wa Kike wa Kanisa la Waadventista nchini humo  ulifanya ziara kwa Rais wa wakati huo na mke wa Rais kujadili masuala yanayowahusu wanawake na familia, pamoja na maeneo ambayo kanisa lingeweza kutoa msaada. Katika mazungumzo ya juma hili, Rais Herminie alihimiza tena viongozi wa kanisa kubainisha njia za vitendo ambazo kanisa linaweza kusaidia jamii, huku Mch Ntep Ntep, akisisitiza kuwa kuimarisha familia kunapaswa kubaki kipaumbele cha msingi katika kukabiliana na changamoto za kijamii.

 Ingawa idadi ya Waadventista nchini Seychelles si kubwa nchini humo, mchango wao katika jamii unaonekana. Kukiwa  na jumla ya waumini 1,116 waliobatizwa hadi Juni 2025. Kuna makanisa 9 na makundi matatu, yaliyosambaa katika visiwa vikuu vya Mahe, Praslin na La Digue. Kwa kuzingatia idadi ya watu wa Seychelles inayokadiriwa kuwa  130,000, takwimu zinaonyesha kuwa mtu 1 kati ya 116 ni Mwadventista. Ukuaji wa kanisa umeendelea kwa utulivu, kutoka wanachama 1,024 mwaka 2018 hadi 1,116 mwaka 2025, sawa na ongezeko la takriban asilimia 9 katika kipindi cha miaka saba.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.