MCHUNGAJI WA WAADVENTISTA AACHIWA NA UHAMIAJI KWA DHAMANA
Luis Morales, mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato mwenye asili ya Venezuela anayehudumu katika Konferensi ya Texas, ameachiliwa kutoka kizuizini na Idara ua Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE), Agosti 19 mwaka huu, baada ya karibu majuma mawili ya kizuizini.
Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya Habari jijini Houston ikiwemo Noticias Telemundo, hakimu anayehusika na maswala ya uhamiaji aliamuru aachiliwe kwa dhamana ya dola za kimarekani 12,000, ambazo marafiki na waumini wa makanisa anayoyaongoza walichangia ambapo pia walikuwa wakimwombea.
Video ya Telemundo inamuonesha Morales akirejea nyumbani akiwa amevalia kifaa cha kielektroniki mguuni na akichukua Biblia yake ili kuomba. Akizungumza baada ya kuachiwa, Morales alitoa shukrani kwa msaada aliopokea na akasema kurejea kwake kwa familia na jumuiya yake ya imani ni jibu la maombi.
Morales alikamatwa Agosti 6 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa George Bush jijini Houston wakati akijiandaa kusafiri na mke wake kwenda New York kuwatembelea binti zao.
Morales ni mchungaji wa makanisa manne ya Waadventista wa Sabato katika jiji la Houston na amehudumu chini ya Konferensi ya Texas tangu Januari 2023. Konferensi ilisema kuwa ana kibali halali cha kufanya kazi na ikaeleza kuwa kujitolea kwake kwa kanisa na familia anazohudumia ni halali.
ICE ilidai kuwa Morales aliingia Marekani kihalali mwaka 2020 lakini alibaki nchini baada ya muda wake wa kukaa kuisha na baadaye hadhi yake ya Hadhi ya Ulinzi wa Muda kwa Wahamiaji(TPS) kumalizika.
TPS ni hadhi maalum inayotolewa na serikali ya Marekani kwa raia wa nchi fulani ambao hawawezi kurudi kwao kwa sababu za vita au machafuko makubwa ya kisiasa, maafa ya asili (kama tetemeko, mafuriko, vimbunga), hali mbaya ya kiusalama au kibinadamu. Watu wanaopewa TPS wanaruhusiwa kuishi Marekani kwa muda fulani, kupata kibali cha kufanya kazi, kutoondolewa nchini Marekani wakiwa na hadhi hiyo. Wakili wake amesema ana kesi ya hifadhi ya kisiasa inayosubiri kusikilizwa.
Morales ameleza kuwa uzoefu wake akiwa kizuizini umeimarisha imani yake na kutegemea Mungu, na akawashukuru waumini na marafiki waliomwombea na kuiunga mkono familia yake. Kuachiwa kwake hakumaanishi mwisho wa kesi yake ya uhamiaji ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kifaa cha mguuni, wakati mchakato wa hadhi ya hifadhi ukiendelea. Kwa sasa, Morales amerudi kwa familia yake na kanisa lake baada ya wafuasi kuchangisha dhamana iliyomwezesha kuondoka kizuizini.
Taarifa za vyombo vya habari za mwaka huu zinaonyesha kuwa wachungaji watatu wamekamatwa na Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) katika jimbo la Texas. Kesi hizi zinajumuisha Mchungaji Luis Morales Pérez na wachungaji wawili wa makanisa ya Assemblies of God Nepthali Zozaya Saucedo na Cinthia Sarai Cardona Otero waliokamatwa katika uwanja wa ndege wa McAllen.
Related Posts
Habari

Post a Comment