MTANGAZAJI

KENYA YAONGOZA DUNIANI KWA MATUMIZI YA AI

 


Kenya inaongoza duniani katika matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI), ikiwa na asilimia 97.5% ya watu wazima wanaotumia intaneti wakitumia teknolojia hiyo kila mwezi.
Ripoti ya masuala ya kidijitali ya nusu ya mwaka 2026 ya dunia , iliyochapishwa na DataReportal kwa ushirikiano na mtandao wa We Are Social na Manochi, iligundua kuwa asilimia 97.5% ya watumiaji wa intaneti waliohojiwa nchini Kenya walitumia angalau kifaa kimoja cha AI mwezi uliopita.
Hiki ndiyo kiwango cha juu zaidi cha matumizi ya AI miongoni mwa nchi 54 zilizofuatiliwa.
Kiwango hiki cha juu kinaendana na juhudi za Kenya za kuhalalisha na kuunda mfumo rasmi wa sekta ya AI, kufuatia kukamilika kwa mchakato wa ukusanyaji maoni ya umma kuhusu rasimu ya Sera ya Kenya ya AI na Teknolojia nyingine zinazoibuka ya mwaka 2026. 
Utafiti wa GWI, uliowahoji zaidi ya watu 240,000 wenye umri wa miaka 16 na kuendelea katika uchumi mkubwa duniani hadi 2026, ulitoa takwimu hizi. Masoko haya yanawakilisha zaidi ya asilimia 80% ya watumiaji wa intaneti duniani.
Kenya ilishika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Falme za Kiarabu (UAE) kwa asilimia 94.2%, na Indonesia kwa asilimia 93.6%.
Matokeo haya yanatofautiana sana na yale ya mataifa makubwa ya Magharibi. Ni asilimia 71.5% tu ya watu wazima wanaotumia intaneti nchini Marekani waliotumia AI katika mwezi uliopita, kiwango kilicho karibu pointi 10 chini ya wastani wa dunia.
Nchini Uingereza, kiwango kilikuwa asilimia 62.8%. Japani ndiyo nchi pekee iliyohojiwa ambapo chini ya nusu ya washiriki waliripoti kutumia AI.
Uongozi wa Kenya unatokea wakati ambapo matumizi ya AI yanaongezeka duniani. Ripoti inakadiria kuwa watu wazima bilioni 4.02, sawa na asilimia 48.6% ya idadi ya watu duniani, sasa wanatumia aina fulani ya AI angalau mara moja kwa mwezi.
Hii inajumuisha zana zilizojengewa ndani ya programu tumishi ikiwemo Microsoft Office, Google Workspace na Canva, pamoja na majukwaa huru ikiwemo ChatGPT.
Matumizi hai ya majukwaa ya generative AI yameongezeka zaidi ya mara mbili katika mwaka mmoja uliopita, yakikua kwa asilimia 141% na kufikia watumiaji bilioni 2.42 duniani.
Waandishi wa ripoti wanabainisha kuwa watumiaji katika nchi za kipato cha chini na cha kati hutumia AI mara nyingi zaidi kuliko wastani wa dunia, ikionyesha kuwa matumizi katika masoko ambayo hayakuhusishwa kwenye utafiti yanaweza kuwa juu zaidi.
Rasimu ya sera ya AI inafuata miezi ya kazi ya kikundi maalum cha kiufundi kilichojumuisha watafiti, serikali, kampuni changa (start-ups) na mashirika ya kiraia.
Mradi huu uliungwa mkono na washirika ikiwemo Kenya ICT Action Network, Ubalozi wa Uingereza, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na Canada.
Rasimu ya sera imejikita katika mkakati wa kitaifa wa Akili Unde 2025–2030,  inaweka muundo wa utawala wa ngazi nne unaoongozwa na Kamati ya kitaifa ya uongozi wa Akili Unde  na teknolojia nyingine zinazoibuka  na baraza jipya la udhibiti.
Inapendekeza kuanzishwa kwa taasisi ya usalama wa AI Kenya  kwa ajili ya majaribio na uainishaji wa hatari, rejesta ya umma, na mpango wa kitaifa wa lugha za kiafrika na sauti  inayolenga kujenga mifumo ya AI inayofanya kazi kwa lugha za kiafrika.
Sera hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwa Baraza la Mawaziri pamoja na mswaada wa AI tofauti ambayo tayari iko mbele ya bunge.
Ripoti inaonya kuwa takwimu za matumizi zinapima tu matumizi ya AI, si kina cha ushiriki na iligundua kuwa sababu kuu ya watu kutumia AI duniani ni kupata taarifa, ikifuatiwa na kutafuta ushauri au kuboresha ujuzi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.