JAJI AONDOA ZUIO LA VISA KWA NCHI 75
Jaji wa shirikisho wa New York, Marekani ameondoa rasmi sera ya utawala wa Rais Donald Trump iliyositisha maombi na utoaji wa visa kwa raia kutoka nchi 75, zikiwemo Afghanistan, Iran, Russia na Somalia. Sera hiyo iliwalenga waombaji ambao serikali ya Donald Trump ilidai kuwa wana uwezekano mkubwa wa kuhitaji msaada wa kijamii wanapowasili Marekani.
Katika uamuzi wake, Jaji Jeannette Vargas, aliyeteuliwa na Rais Joe Biden, amesema sera hiyo ilikuwa kinyume cha sheria na imezidi mamlaka ya kisheria ya serikali. Jaji Vargas amebainisha kuwa Waziri anayehusika na Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alizidisha mamlaka yake kwa kutoa sera inayowazuia waombaji visa bila msingi wowote wa kisheria, na kwamba hatua hiyo inakiuka Sheria ya Uhamiaji na Utaifa.
Jaji huyo amesema maafisa wa ubalozi ndio wanaopewa na Bunge mamlaka ya kufanya maamuzi ya visa kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyowekwa kisheria. Ameeleza kuwa sera hiyo inayokataza visa kwa misingi ya uraia wa mwombaji ni uvunjaji wa moja kwa moja wa mfumo wa kisheria uliowekwa na Bunge.
Sera hiyo ilipingwa na mashirika mawili yasiyo ya kiserikali pamoja na watu 11, wakiwemo wale ambao jamaa zao walikataliwa visa. Mashirika hayo yamesema uamuzi wa mahakama ni ushindi mkubwa kwa familia zilizotenganishwa na sera hiyo.
Anna Gallagher, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la CLINIC, amesema uamuzi huo unarejesha matumaini kwa familia ambazo zilikuwa zimekwama kwa muda mrefu. Amesema mafundisho ya kijamii ya Kanisa Katoliki yanasisitiza utu wa binadamu na umuhimu wa familia kama msingi wa jamii.
Shirika la African Communities Together, lililoko Harlem, pia limepongeza uamuzi huo, likiuita ushindi mkubwa kwa utawala wa sheria. Diana Konate, mmoja wa viongozi wa shirika hilo, amesema marufuku hiyo iliwadhuru watu bila kipimo na kuwatenganisha familia kwa ukatili.
Sera hii ilikuwa sehemu ya mpango mpana wa utawala wa Trump wa kupanua vikwazo vya uhamiaji, hasa kwa raia kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Wakati sera hiyo ilipotolewa, Wizara ya Mambo ya Nje ilielekeza maafisa wa ubalozi kusimamisha maombi ya visa za wahamiaji kutoka nchi 75 kwa misingi ya amri iliyolenga watu ambao huenda wakawa mzigo wa kijamii.
Uamuzi huu ni mfululizo wa maamuzi ya mahakama yanayopinga sera za uhamiaji za utawala wa Trump. Mwezi Juni, jaji mwingine alibatilisha sera iliyofanya iwe vigumu kwa wahamiaji kutoka nchi nyingi kuingia na kubaki Marekani, ikihusisha maombi ya hifadhi, vibali vya kazi, kadi za kijani na hata uraia.

.png)
Post a Comment