MTANGAZAJI

MKAKATI WA ONEVOICE27 WA WAADVENTISTA ULIMWENGUNI




Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni liko katika utekelezaji wa mpango mkakati wa kimataifa wa uinjilisti wa kidijitali unaoitwa OneVoice27, mpango unaoratibiwa na Konferensi Kuu ya Kanisa hilo na kutekelezwa katika divisheni zote 13  duniani. 

Lengo kuu ni kuunganisha sauti za Waadventista ikiwemo wachungaji, wazee, vijana, waimbaji, waandishi, wataalamu wa vyombo vya habari, na washiriki wa kawaida ili kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kufikisha injili kwa watu milioni 27.

OneVoice27 ni mkakati wa uinjilisti, si mradi wa vyombo vya habari pekee. Unahimiza kila mshiriki kutumia kipawa chake kutengeneza maudhui, kutafsiri, kuchapisha, au kushiriki ujumbe wa injili mtandaoni. Mpango huu unalenga kuwafikia watu ambao huenda hawafiki kanisani, lakini wanapatikana mtandaoni. Unasisitiza kuwa kila jukwaa la kidijitali ni mimbari, na kila simu janja ni chombo cha uinjilisti.

Viongozi wa Kanisa hilo wanasema mafanikio ya uinjilisti wa kidijitali hayapimwi kwa likes au views, bali kwa safari ya mtu kutoka mawasiliano ya mtandaoni, hadi shauku ya kiroho, masomo ya Biblia, kuunganishwa na kanisa, na hatimaye kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo.

Mpango wa OneVoice27 tayari umezinduliwa katika maeneo mbalimbali duniani, ambapo Afrika kumekuwa na utekezaji mkubwa ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini,  Angola, Botswana, Msumbiji, Madagascar, Mauritius, Seychelles, Kenya, Uganda, Zambia, na Malawi kutokana na kuwa na watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii hasa vijana.

Uzinduzi katika divisheni nyingine unaendelea, kuelekea kilele cha kimataifa cha uinjilisti wa kidijitali mnamo Septemba 2027, ambapo makanisa na washiriki duniani kote wataungana katika kampeni za pamoja za kufikisha injili kupitia majukwaa ya kidijitali. Septemba 2027, inakisi  kumbukumbu ya miaka 2,000 tangu ubatizo wa Yesu Kristo. Kanisa la Waadventista wa Sabato duniani kote litamtangaza Masihi kwa pamoja, katika kila taifa, kupitia kila aina ya chombo cha mawasiliano.

Kwa sasa, Kanisa la Waadventista wa Sabato  linahimiza kila mshiriki kutumia teknolojia kuwa uwanja wa utume, ili sauti moja ya injili ifike mbali zaidi kupitia OneVoice27.



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.