MTANGAZAJI

WAADVENTISTA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTEKELEZA MIRADI YA AFYA NCHINI GHANA.

 


Taasisi za huduma za Afya za Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Ghana (GAHS) zimeonyesha utayari wa kushirikiana na serikali kukamilisha baadhi ya miradi ya afya ya Agenda 111 nchini humo. Ahadi hiyo ilitolewa baada ya ujumbe wa Kanisa la Waadventista, ukiongozwa na Dkt. James Antwi, kukutana na Waziri wa Afya nchini humo, Kwabena Mintah Akandoh, hivi karibuni.
 
Ujumbe huo uliwasilisha pendekezo linalolenga maeneo manne muhimu ambayo ni huduma za majeruhi na dharura, ustawi wa mwili na akili, matibabu ya saratani, na huduma za urekebishaji na afya. Lengo ni kulifanya Kanisa la Waadventista kuwa mshirika wa kimkakati katika kuboresha utoaji wa huduma za afya, hasa katika maeneo yasiyohudumiwa vya kutosha.
 
Waziri wa Afya nchini Ghana alilipokea pendekezo hilo kwa moyo mkunjufu na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mashirika ya kidini na sekta binafsi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya nchini Ghana.

Mtandao wa GAHS unajumuisha zaidi ya taasisi 40 za afya na vyuo saba vya mafunzo, huku orodha rasmi ya Waadventista ikionyesha hospitali na vituo vya Afya vya kanisa hilo  katika maeneo mbalimbali ya nchini Ghana.
 
Alihimiza Umoja wa Kikiristo wa watoa huduma za afya nchini Ghana (CHAG) na taasisi za sekta binafsi kubaini miradi mahususi ya Agenda 111 ambao wako tayari kuisaidia na kushirikiana na serikali katika kukamilisha na kuiendesha.
Bw. Akandoh aliwahakikishia washirika watarajiwa kwamba serikali itatoa mwongozo unaohitajika ili kuwezesha kukamilika kwa miradi hiyo.
 
Alifafanua kuwa ushirikiano unaopendekezwa hautahitaji washirika kutoa fedha moja kwa moja kwa serikali, bali kutoa msaada wa kukamilisha vituo vya afya vilivyochaguliwa.
 
Waziri alilitoa shukrani kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa mchango wake katika utoaji wa huduma za afya, hasa katika maeneo yasiyohudumiwa vya kutosha, na kwa utayari wake wa kuunga mkono ajenda ya afya ya serikali.
 
Mpango wa Agenda 111, uliozinduliwa chini ya Rais wa zamani Nana Addo Dankwa Akufo-Addo, uliundwa kwa lengo la kujenga hospitali 111 kote nchini humo, ikiwemo hospitali 104 za wilaya, saba za mikoa na vituo vya afya ya akili.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.